Friday, September 27, 2013

Bodi ya mikopo yatangaza wanafunzi waliopata mikopo elimu ya juu



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
Serikali katika mwaka wa masomo wa 2013/14 imewapangia mikopo wanafunzi wa elimu ya juu 29,754 sawa na aslimia 94.04%  katika malengo yake ya kuwakopesha wanafunzii 31,647.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Bw. Cosmas Mwaisobwa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumzia utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na elimu ya juu.

“Uchambuzi wa maombi ya mikopo kwa mwaka huu wa masomo umekamilika,”na aliongeza kusema lengo la serikali ni kuwawezesha wanafunzi wa elimu ya juu kwa muda muafaka.
Alisema kuwa mchanganuo wa utuoaji wa mikopo hiyo ulizingatia vigezo na masharti ya uombaji mikopo na ruzuku.

Alisema kuwa idadi ya waombaji wapya waliotuma maombi ya mikopo ni 53,239, waombaji wanaoendelea na masomo 43,032, waombaji waliokuwa na maombi yenye matatizo ni 6,364.

“Wengine ni  waombaji waliorekebisha matatizo kwenye maombi yao 3,151 na waombaji ambao hawakurekebisha matatizo kwenye maombi yao 3,213”, alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu mchanganuo huo alisema waombaji wapya 53,630 watakaosoma  ndani na nje ya nchi wamepata mikopo hiyo.

Alisema maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea 61,692 ambao wanasoma ndani na nje ya nchi wamepangiwa kupata mikopo hiyo.

Bodi ya mikopo ya elimu ya juu inatarajia kutoa mikopo ya sh.306 bilioni kwa ajili ya ukopeshaji wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.

Alisema mchakato wa upangaji wa mikopo unaendelea vizuri ambapo hadi sasa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

“Matarajio ni kukamilisha mchakato huu kwa asilimia 100 ifikapo wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba kabla ya Vyuo vya Elimu ya Juu kufunguliwa, kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu”, alisema.

Aliongeza kusema orodha kamili ya waombaji wapya waliopangiwa mikopo inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) ambapo mwombaji anaweza kutafuta jina lake kwa kutumia namba ya mtihani ya kidato cha nne.

Alisisitiza kuwa taratibu za kupeleka mikopo yao vyuoni zinaendelea na kwamba watalipwa baada ya kufanya usajili.

Aidha, ailisistiza umuhimu wa kila mwombaji kuwa na akaunti ya benki kwa ajili ya kupitishia mikopo hiyo.

Aliongeza kusema kuwa waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo wanawajibika kurejesha mikopo hiyo baada ya kuhitimu masomo yao. 

Mwisho.

Thursday, September 26, 2013

Serikali yawahakikishia wawekezaji, sekta binafsi ushirikiano zaidi



Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kushoto) akiongea na Gavana wa kisiwa cha Anjouan, Comoro, Anissi Chamsidine (kulia) wakati wa kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini jana mjini Tanga.  Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Chiku Gallawa (wa pili kulia aliyesimama), afisa wa Anjouan, Bw. Allaoui Toihirdine (katikati aliyekaa) na Naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Aggrey Mwanri (wa pili kushoto).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bi. Juliet Kairuki (kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Fedha, Bi. Saada Mkuya Salum wakati wa kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini jana mjini Tanga.  Kongamano hilo la siku mbili limetayarishwa na TIC.

Na Mwandishi wetu, Tanga
Serikali imesema kuwa inatambua mchango wa sekta binafsi katika kufikia maendeleo na kwamba itaendelea kuweka mazingira yanayofaa kuiwezesha kutumia fursa za uwekezaji hapa nchini.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo alipokua akifungua kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini lililoanza jana mjini Tanga.
Waziri Mkuu alisema mchango wa sekta binafsi na wawekezaji hasa wale wa ndani ni mkubwa sana na serikali inaendelea kujenga mazingira bora ili uwekezaji uwe rahisi zaidi kwa faida ya pande zote mbili.
“Nitakuwa mtu wa mwisho kudhihaki mchango wa sekta binafsi hasa ya ndani katika maendeleo ya nchi hii,” alisema.
Alisema sekta hiyo na wawekezaji watumie fursa ya mazingira bora yanayojengwa na serikali kuhakikisha wanafanya kazi na kuendelea huku akiitaja sera ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma (PPP) kama moja ya firsa hizo.
Alisifu Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa juhudi ilizochukua kuratibu kongamano hilo la kanda ya kaskazini na kutangaza fursa zake ambazo amesema bado hazijatumiwa vya kutosha.
Alieleza kuwa kongamano kama hizo ni muhimu sana katika kuwasiliana na wawekezaji na kuangalia jinsi wanavyoweza kushirikiana na serikali kuleta maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary nagu alisema uwekezaji ni njia moja wapo muhimu katika kugeuza fursa kuwa na kuwa maendeleo.
Alitoa wito kwa viongozi wa mikoa katika kanda hiyo ya kaskazini kuhakikisha kuwa wanashughulikia pia maendeleo ya uchumi na uwekezaji katika maeneo yao ili kuleta mapinduzi ya uchumi haraka.
“Hii itasaidia kufikia maendeleo kwa haraka zaidi,” alisema.
Akiwasilisha mada kuhusu fursa zinazopatikana katika kanda ya kaskazini, mhadhiri mwandamizi toka Taasisi ya Maendeleo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Suleiman Ngware alisema wawekezaji wawe na uhakika wa faida wanapokuja Tanzania kwa sababu ya amani na utengamano wa kitaifa uliopo.
“Pamoja na amani, kanda hii na nchi nzima ina raslimali za kutosha na fursa mbalimbali kwa wawekezaji,” alisema.
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Bi. Chiku Gallawa alikaribisha wawekezaji katika mkoa wake na kanda ya kaskazini  na kuwahimiza kutumia fursa.
“Tunawahakikishia ushirikiano mkubwa,” alisema.
Kongamano hilo la siku mbili lilivutia wawekezaji zaidi ya 1,500 linahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi, viongozi wa dini, mabalozi na wadau wengine wa maendeleo.
Pia, Gavana wa kisiwa cha Anjouan, moja ya visiwa vinavyounda nchi ya Comoro, Anissi Chamsidine anahudhuria kongamano hilo.
Mikoa inayounda kanda ya kaskazini ni pamoja na Tanga, Manyara na Arusha.
Baadhi ya vivutio katika kanda ya kaskazini ni ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao ya biashara, mbogamboga na matunda, madini, na utalii.
Mwisho

Wednesday, September 25, 2013

Watanzania watakiwa kuchangamkia fursa kuwekeza Anjouan



Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bi. Juliet Kairuki (kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara ya Gavana wa kisiwa cha Anjouan Bw. Anissi Chamsidine katika kituo hicho jana jijini Dar es Salaam.  Gavana huyo yuko nchini kwa ziara ya wiki moja.  Katikati ni mke wa Gavana huyo, Bi. Laouya Shamsidine.



Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bi. Juliet Kairuki (katikati) akimkabidhi zawadi ya picha Gavana wa kisiwa cha Anjouan Bw. Anissi Chamsidine (kulia) ambaye yupo nchini kwa ziara ya wiki moja.  Gavana huyo alitembelea kituo hicho jana.  Kushoto ni mke wa Gavana, Bi. Laouya Shamsidine.


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.

Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika kisiwa cha Anjouan nchini Comoro ili kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo kwa maslahi ya kijamii na kiuchumi kati ya pande hizo mbili.

Gavana wa Anjouan, Bw Anissi Chamsidine alieleza hayo alipotembelea Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jana jijini Dar es Salaam.

“Tuna fursa nyingi za uwekezaji katika kisiwa cha Anjouan na tunaamini watanzania wako katika nafasi nzuri ya kuzitumia,” alisema na kuongeza kuwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili ni wa damu na wa kihistoria.

Alisema kuwa kuna unmuhimu wa kuendelea kushirikiana katika eneo la uwekezaji na kutaja maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji kuwa ni elimu, utalii, nishati na katika sekta ya afya.

“Tuna hospitali kubwa zinajengwa lakini tatizo ni kukosekana kwa wataalamu wa afya ikiwemo wauguzi na madaktari hivyo tunaomba watanzania waje kutusaidia katika eneo hilo,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bi. Juliet Kairuki amesema kuwa ujio wa Gavana huyo na ujumbe wa wawekezaji utasaidia kufungua fursa za uwekezaji na ushirikiano mzuri kiuchumi kati ya nchi hizo.

“TIC na serikali inathamini ziara ya Gavana na ujumbe wake, mahusiano yetu ni ya siku nyingi na tungependa kuyaimarisha,” alisema na kuongeza kuwa ziara hiyo itasaidia kuvutia uwekezaji kutoka katika kisiwa hicho.

Kama moja ya ratiba zake akiwa hapa nchini, Gavana huyo anatarajiwa kushiriki katika kongamano kubwa la uwekezaji kanda ya kaskazini linalotarajiwa kuanza mkoani Tanga asubuhi hii.

Benki mbalimbali, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (EPZA) na Muungano wa wenye viwanda Tanzania (CTI) ni baadhi ya walioalikwa kwenye kongamano hilo.

Kongamano hilo linatarajia kuvutia washiriki 1,500 toka ndani na nje ya nchi, ikiwemo China.

Baadhi ya vivutio katika kanda ya kaskazini ni ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao ya biashara, mbogamboga na matunda, madini, na utalii.

Gavana huyo atakutana pia na wakuu wa mikoa inayounda kanda hiyo ya kaskazini, mmoja mmoja wakati wa kongamano hilo.

Mratibu wa ziara hiyo kwa upande wa Anjouan, Bw. Allaoui Toihirdine alisema kuwa mahusiano ya Anjouan na Tanzania ni ya kihistoria na kwamba ziara hiyo itaimarisha uhusiano huo.

Alisema, Anjouan inatambua mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania katika kukikomboa kisiwa hicho mwaka 2009 na kukirudisha katika utawala wa muungano wa visiwa vya Comoro.
Mwisho