Tuesday, May 6, 2014

Wafanyabiashara DRC wapata matumaini ofisi ya TPA Lubumbashi

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto) akimueleza jambo Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba wakati wa uzinduzi wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi katika jimbo hilo hivi karibuni.  Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Madeni Kipande (kulia).
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto) na Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba wakifuatilia jambo wakati wa uzinduzi wa ofisi ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi katika jimbo hilo hivi karibuni.  Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Madeni Kipande (kulia).
Sehemu ya wafanyabiashara wa DRC Congo waliohudhuria uzinduzi wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni.  Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Harrison Mwakyembe kusaidia wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akisaini kitabu cha wageni katika ofisi mpya ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni.  Wanaoshuhudia ni Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba (kushoto) na mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bi. Zarina Madabida (kulia).
Na Mwandishi wetu, Lubumbashi

Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) wamesema wana matumaini makubwa na hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga nchini humo.

Wakiongea kwa niaba ya wenzao baada ya kuzinduliwa kwa ofisi hiyo hivi karibuni, wafanyabiashara hao wanaopitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam, wamesema kuanzishwa kwa ofisi hiyo kumekuja wakati muafaka na kuwa itawarahisishia biashara yao.

Sasa wafanyabiashara hao wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa.

Mmoja wa wafanyabishara hao, Bw. Mubanzo Fils anayeendesha kampuni ya ETS Mubanzo alisema jumuiya ya wafanyabiashara Lubumbashi imefurahia sana kupata ofisi hiyo wanayotarajia kurahisisha kazi zao na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.

“Tuna furaha kubwa sana kwa hatua hii muhimu,” alisema.

Inatarajiwa kwamba tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.

Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.

Kwa upande wake, Bw. Lumbu Useni wa kampuni ya Luwang SPRL alitoa wito kwa wafanyakazi kwenye ofisi hiyo ili kutimiza lengo lilikusudiwa.
“Wafanye kazi kwa bidii na akili zao zote ili lengo lililokusudiwa na nchi hizi lifikiwe na sisi tuweze kufaidika,” alifafanua.

Mizigo ya DRC inayopita katika bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

Nchi hiyo ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.

Mfanyabiashara mwingine, Bw. Mohamed Hassan Hammy, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Drill Tek ya mjini humo alisema Kongo ni soko kubwa hivyo Tanzania imefanya busara kubwa kufungua ofisi hiyo.

Bw. Hammy ambaye ni mtanzania alisema pamoja na kwamba kufungua ofisi hiyo ya TPA ni hatua kubwa, jumuiya ya wafanyabiashara mjini hapo wanaomba serikali kufungua ofisi ndogo ya ubalozi wa Tanzania Lubumbashi ili kuwasaidia katika mambo yao mbalimbali.

“Tunaipongeza serikali kufungua ofisi hii ya TPA lakini pia tunaiomba ifungue ubalozi mdogo hapa Lubumbashi ili kutusaidia sisi watanzania tunaoishi hapa,” alisema, na kuongeza kuwa kwa sasa wanalazimika kusafiri umbali wa kilometa 2,000 hadi mjini Kinshasa wanapohitaji huduma za ubalozi wa Tanzania.
“Kinshasa ni mbali sana na ni gharama kubwa,” alifafanua.

Awali, Waziri ya Uchukuzi wa jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba alisema ufunguzi wa ofisi hiyo sio tu utarahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam, bali pia utasaidia kuboresha maisha yao.

“Kurahisisha biashara ina maana ya kupata maendeleo na kuboresha maisha yetu, tunaishukuru sana serikali ya Tanzania kwa uamuzi huu,” alisema baada uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Aliihimiza jumuiya ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuthibitisha kuwa kweli walikuwa wanaihitaji ofisi hiyo kwa kuitumia kutatua matatizo yao.

“Thibitisheni kwa vitendo kuwa kweli mlikuwa mnaihitaji ofisi hii,” aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika tukio hilo la uzinduzi.  


Mwisho

Monday, May 5, 2014

DRC yaisifu Tanzania kwa kufungua ofisi ya TPA Lubumbashi

Na Mwandishi wetu, Lubumbashi

Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) imesema hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) ni ya kizalendo na inayothibitisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo.

Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni baada ya uzinduzi wa ofisi hiyo mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga, Waziri ya Uchukuzi wa jimbo hilo, Bw. Kahozi Sumba alisema ufunguzi wa ofisi hiyo sio tu utarahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam, bali pia utasaidia kuboresha maisha yao.

“Kurahisisha biashara ina maana ya kupata maendeleo na kuboresha maisha yetu, tunaishukuru sana serikali ya Tanzania kwa uamuzi huu,” alisema baada uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Waziri Sumba alisema kuwa sasa serikali inatarajia kuwa wafanyabiashara wa Kongo hawatakumbana tena na changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo awali katika biashara zao kati ya Kongo na Tanzania kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Aliihimiza jumuia ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuthibitisha kuwa kweli walikuwa wanaihitaji ofisi hiyo kwa kuitumia kutatua matatizo yao.

“Thibitisheni kwa vitendo kuwa kweli mlikuwa mnaihitaji ofisi hii,” aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika tukio hilo la uzinduzi.   
Awali, akiongea kwa niaba ya Gavana wa jimbo la Katanga, Bw. Moise Katumbi; Naibu Gavana wa jimbo hilo, Bw. Yav Guilbert alimmwagia sifa Waziri Mwakyembe akisema waziri huyo amethibitisha kuwa ni mtu wa vitendo.

Katika ziara yake mwezi Machi mwaka huu mjini Lubumbashi, Waziri Mwakyembe aliahidi kuwa ofisi hiyo ingekuwa tayari mwishoni mwa mwezi Aprili, jambo ambalo limetekelezwa kwa wakati.

“Waziri Mwakyembe si aina ya wanasiasa wanaotoa ahadi za uongo na ameonyesha kuwa Tanzania inaweza kuileta Afrika pamoja na kupata maendeleo,” alisema.

Awali, Dk. Mwakyembe alisema kuwa ofisi hiyo mpya itasaidia wafanyabiashara wa DRC kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.

“Wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.

Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.

Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara tokea Dar es Salaam hadi Lubumbashi kupitia Zambia kwa barabara zaidi ya kilometa 2000 kuangalia na kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC kuanzia bandarini Dar es Salaam hadi njiani wanaposafiri.

Ofisi ya Lubumbashi inalenga kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabishara hao zikiwemo ucheleweshaji, wizi, vikwazo visivyohusiana na kodi na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu.

“Juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa vikwazo na urasimu wote unaowakabili wafanyabiashara wa DRC unakwisha,” alifafanua Waziri.
Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.

Pamoja na maafisa wengine, ujumbe wa Tanzania Lubumbashi ulijumuisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba, mjumbe wa kamati hiyo, Bi. Zarina Madabida, maafisa waandamizi toka TPA, Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), Tanzania Railways Limited (TRL), TAZARA na wengine.

Mwisho


Maghembe ajivunia maendeleo ya sekta ya elimu Mwanga

Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari, hawapo pichani,akielezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta ya elimu  na afya katika katika jimbo lake, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua shughuli za maendeleo  hivi karibuni.
Waziri wa Maji ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Profesa Jumanne Maghembe katikati akitoa maelekezo kwa fundi ujenzi, Bw. Norbert Abraham ( kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika sekta za elimu na afya katika wilaya ya Mwanga  hivi karibuni, kushoto ni Diwani wa kata ya Kileo Bw. Kuria Msuya.
Na Mwandishi wetu, Mwanga
Wilaya ya Mwanga  Mkoa wa Kilimanjaro imeelezwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuinua sekta hiyo.

Waziri wa maji ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa ushirikiano uliojengeka katika ya sekta ya uma na binafsi umechangia mafakio ya elimu katika wilaya hiyo.

“Nina furaha kusema kuwa Wilaya ya Mwanga imepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu,”Prof. Maghembe alipotakiwa na waandishi wa habari kuelezea maendeleo ya elimu jimboni kwake.

Prof. Maghembe  alisema  katika ngazi h ya msingi mwaka huu watoto walifaulu kwa  asililia 65 lakini mwaka uliopita kabla ya mwaka 2012 watoto wa Mwanga walifaulu kwa  asilimia 95.

“Wakati nachuku jimbo hili mwaka 2000, wilaya hii ilikua na shule za msingi 93 tu, lakini hadi kufikia sasa tunashule zipatazo 118 haya ni mafanikio makubwa sana”, alisema na kuongeza kuwa  ujenzi zaidi wa shule unaendelea.

Prof. Maghembe alisema kwa muda wa miaka kumi mfululuzo, Wilaya ya Mwanga kwenye matokeo ya shule za msinginimekuwa katika kapu la kumi bora ‘top-ten’ katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wa  shule za sekondari mpaka sasa, Waziri Maghembe alisema shule  zipo 25 na hivyo kufanya angalau kila kata katika wilaya hiyo kuwa na shule ya sekondari, japo zipo baadhi ya kata zina shule mbili mpaka tatu kulingana na juhudi kubwa za wananchi wa kata husika.
 “ lengo la serikali ni kwamba kila wilaya itakua na shule moja yenye kidato cha kwanza mpaka cha sita katika kila tarafa, hapa mwanga malengo hayo yametimizwa katika tarafa zetu tano,”alisema

“ Mchango wa sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya elimu katika jimbo hili ni mkubwa sana na mpaka sasa  kuna shule za sekondari zaidi ya 16 katika Wilaya ya Mwanga,” alisisitiza.

Naye Diwani wa kata ya Kileo, Bw. Kuria Msuya alisema uhamasishaji  mkubwa uliofanywa na Prof. Maghembe umeleta chachu katika upatikanaji wa mafanikio makubwa kwenye sekta ya elimu wilayani Mwanga..

“ Mimi kama diwani wa Kileo nasema kata yangu inatoa kipaumbele kikubwa katika elimu na mbunge wetu yupo nyuma kuunga mkono jihada zetu na mafanikio yanaonekana na mwenye macho haambiwi aone,” alisema Bw. Msuya.

  Alisema mbali ya elimu, Bw. Msuya alisema ukaribu unaaonyeshwa na Profesa Maghembe umeleta mafanikia makubwa  katika sekta nyingine mbalimbali muhimu katika wilaya Mwanga,

“ Tumepiga hatua  katika eneo la afya, elimu, miundo mbinu na sasa suala la maji linatekelezwa kwa kasi kuhakikisha maji yanakua ya kutosha hapa mwanga,”alisema Bw. Msuya na kuongeza kuwa wanamwanga wana matumaini makubwa na mbunge wao.

Naye  Bi. Ingia Yoel , mkazi wa Mwanga mjini alisema anashukuru kwa kuwepo na  vituo vingi vya afya katika wilaya hiyo na kuongeza kua kwa sasa suala la afya limepata suluhisho la kudumu kutokana na huduma kuwa karibu na wananchi.

“ Akina mama kwa sasa tumepata ahueni ya kutembea mwendo mrefu kupata huduma za afya, vituo vipo karibu sana na wananchi,”alisema Bi. Ingia na kumshukuru sana WMaghembe.. 
                                                             
Mwisho.