Sunday, September 15, 2013

Nafasi ya vyuo vikuu katika Matokeo Makubwa Sasa yasisitizwa








Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Prof. Sylivia Temu (katikati) akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawalana Fedha, Prof. Faustin Kamuzora (kulia) wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha mwishoni mwa wiki.  Kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) ambao ndio walitayarisha kongamano hilo.




Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawalana Fedha, Prof. Faustin Kamuzora (kulia) akiongea jambo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Magishi Mgasa wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha mwishoni mwa wiki.  Kongamano hilo lilitayarishwa na jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT).

Na Mwandishi wetu, Arusha
Wasomi nchini wamesisitiza umuhimu wa taasisi za elimu ya juu katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati kabambe wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa.
Mkakati huo uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Februari mwaka huu unalenga kufikia malengo katika vipaumbele vya maendeleo ya nchi kwa muda maalum ambapo viongozi watatakiwa kuonyesha walichofanikisha.
Akizungumza wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha mwishoni mwa wiki, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawala na Taaluma, Prof. Faustin Kamuzora alisema kuwa vyuo vikuu vinafanya kazi na serikali na sekta za wazalishaji ambao ni watekelezaji wakubwa wa mkakati huo.
Alisema Mkakati huo wa Matokeo Makubwa Sasa ni muhimu sana kwa kuwa baadhi ya ajira zitakazozalishwa kutokana na utekelezwaji wake zitachukuliwa na wahitimu wa vyuo vikuu.
“Ni kwa faida ya vyuo vikuu kuhakikisha mpango huu unafanikiwa kwa faida ya nchi na pia kuwapatia ajira nzuri wahitimu wake,” alisema.

Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu uliotayarishwa na jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) ni jinsi gani vyuo vikuu vinaweza kushirikiana na waajiri ikiwemo viwanda na makampuni ili kujenga elimu ya juu endelevu Tanzania.
Vipaumbele vya mkakati huo wa serikali ni pamoja na elimu, nishati, kilimo, usafiri, maji na maendeleo ya raslimali watu.
Katika sekta ya elimu, mkakati huu unalenga kuongeza ufanisi katika ngazi za chini za elimu za chekechea, shule za msingi na sekondari.
Katika sekta hii, mkakati huo unalenga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2013, asilimia 70 mwaka 2014 na asilimia 80 mwaka 2015.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Prof. Sylivia Temu alisema kuwa taasisi za elimu ya juu zina wajibu kuhakikisha kuwa mkakati huo unafanikiwa.
“Ni muhimu kwa vyuo vikuu kuhakikisha mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa unafanikiwa kwa kuzalisha walimu wenye uwezo,” Prof. Temu aliyekuwa anaongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo alisema.

Alisema pia vyuo hivyo vijiweke tayari kupokea wanafunzi toka shule za sekondari watakaoongezeka kutokana na mkakati huo.

Alitoa mfano kuwa wakati serikali inahitaji walimu 25,000 wa sayansi, inazalisha walimu 2,000 pekee kwa mwaka.

“Hiyo ni changamoto kwa taasisi za elimu ya juu…ni lazima itafutiwe ufumbuzi kama kwali tunataka kufanikiwa katika utekelezaji wa mkakati huu,” alisema.

Lengo kubwa la CVCPT ni kukutanisha wadau wa elimu ya juu kwa upande mmoja na wadau wengine wa maendeleo nchini kwa lengo la kujadiliana jinsi ya kuimarisha elimu ya juu na raslimali watu hapa nchini.
CVCPT ilianzishwa mwaka 2005.
Wajumbe wa CVCPT ni makamu wakuu wa vyuo vikuu pamoja na wakuu wa taasisi za elimu binafsi na vya umma pamoja na katibu mtendaji wa TCU.
Kama mwenyekiti wa sasa wa CVCPT, Chuo kikuu Mzumbe kimekua kikitayarisha kongamano hilo kwa mwaka wa pili mfululizo sasa.


Mwisho.

TPSF yawapa changamoto Vijana kuwa wabunifu,kutumia fursa ili kujiendeleza kuichumi



Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) imewataka vijana nchini kuwa wabunifu na kutumia fursa za kibiashara ili kukuza vipato vyao na pato la taifa.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bw. Reginald Mengi alisema hayo wakati wa hafla ya kumkabidhi  tuzo ya heshima Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Helvetic Solar Contractors LTD, Mhandisi, Patrick Ngowi jijini, Dar es Salaam mwishoni mwa juma kama njia ya kutambua mafanikio aliyoyapata katika biashara.
“Vijana wanawajibu wa kutumia vipaji vyao na elimu kujiendeleza kibiashara ili waweze kukua kibiashara na kulisaidia taifa kuboresha ustawi wa jamii,”alisema.
Alisema kijana aliyetunukiwa tuzo hiyo ameweza kufanikiwa kibiashara akiwa na umri wa miaka 28, hivyo vijana wengine wanatakiwa kuiga mfano huo.
Alisema taifa linategemea vijana hivyo wanatakiwa kujituma ili waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa na matajiri wasaidie jamii inayowazunguka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema kijana huyo amefanikiwa kupitia biashara ya ukandarasi wa kutumia teknolojia ya nishati ya jua (Solar Power contractor) kusambaza umeme.
“Kijana huyu kwa sasa anamiliki makampuni mbalimbali ya kusambaza na kutumia nishati ya jua katika nchi tatu za Afrika Mashariki,”
Alisema makampuni hayo yamejumuishwa kundi la makampuni ya Helvetic Group of Companies lenye jumla ya mapato ya mamilioni ya dola.
“Mwaka 2011 kampuni hizi zilikuwa na pato la sh. Bilioni 12 na mwaka huu inatarajia kufikia pato la bilioni 20,”
Aliongeza kusema kwamba TPSF imempatia tuzo hiyo kwa kutambua juhudi zake kibiashara na kupata tuzo mbalimbali za kimataifa kama mjasirimali mdogo.
Pia kupitia tuzo za kimataita alizopata, ameweza kuitangza nchi nje ya nchi kwamba watanzania wanaweza.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Regina Kikuli ambaye alimkabidhi tuzo kijana huyo alisema tuzo hiyo iwe ni chachu kwa kijana huyo kuzidi kupata mafanikio zaidi.
“Serikali inaendelea kujenga mazingira mazuri kwa wajasirimali na wawkezaji ili nchi izidi kukua kiuchumi,”
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Helvetic Solar Contractors LTD, Mhandisi Patrick Ngowi vijana wasikate tamaa wajitume na kutumia fursa zilizopo.
“Mimi nilianza nikiwa sina kitu niliona fursa nikakopa fedha kisha nikaanza kufanya biashara na leo nimefikia hapa,” alisema.
Tuzo hiyo iliandaliwa na TPSF kwa kutambua mafanikio ambayo kijana huyo ameyafikia kibiashara.
Mwisho.

Dkt. Turuka: Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji




Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dtk Florens Turuka akielezea nia ya serilakali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara hapa nchini kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma.
 


Na Mwandishi wetu
Serikali imewahakikishia wawekezaji kuwa itaendelea kuweka mazingira bora  ya kufanya biashara na uwekezaji kama chachu ya  kuvutia zaidi uwekezaji  hapa nchini ilikuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji  wa uchumi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yatasaidia kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na huduma.
“Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sera na sheria” ambazo zinatoa fursa kwa wawekezaji kufanya shughuli zao bila vikwazo vyovyote hapa nchini,” alisema Dkt.Turuka.
Aliongeza kwa kusema kuwa serikali imeidhinisha mpango wa maboresho wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji unaoainisha maeneo kumi yanayolenga taratibu za kisera,kisheria na za kiutawala zinazozingatiwa na wafanyabiahsra na wawekezaji.
Akisisitiza zaidi, Dkt. Turuka alisema, kuanzia mwaka 2003 hadi sasa serikali imefanya maboresho mbalimbali yakiwemo ya taasisi zake kufanya kazi kwa ubunifu na ushirikiano ili kuleta tija na ufanisi zaidi.
Akitolea mfano Bandari ya Dar es Salaam alisema huduma zote za ukaguzi wa ubora wa bidhaa kutoka nje ya nchi zinafanyika bandarini na zinahusisha mamlaka zote muhimu.
“Kwa mfano shughuli za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine zinafanyikia bandarini hapo ikiwa ni moja ya mikakati ambayo serikali imechukua katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara”, Dkt. Turuka alisema.
Pia alisema muda wa kusajiri kampuni na kupata vibali mbalimbali hutolewa kwa muda mfupi sana ikilinganishwa na siku za hapo nyuma.
“Vituo vya ukaguzi wa mizigo barabarani vimepunguzwa kutoka hamsini hadi 15 ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoenda nje ya nchi,” alisema Dkt.Turuka na kuongeza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara.
Mifumo ya ulipaji kodi inafanyika kwa njia rahisi za kieletroniki katika malipo ya kodi mbalimbali kwa kutumia simu za mkononi ili kupunguza gharama na usumbufu kwa wafanyabiashara kupata huduma zote za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pamoja na Tanzania kufanya maboresho hayo, mashirika kimataifa ikiwemo Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Biashara (UNCTAD), Kongamano la Uchumi Duniani (WEF) na Benki ya Dunia (WB) yanasema Tanzania inahitaji kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Sisi kama Serikali tutaendelea kutumia tathimini zilizotolewa na mashirika hayo kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini na kufikia matarajio ya wafanyabiashara na wawekezaji,” alisema Bw. Turuka.
Alisisitiza kuwa maboresho hayo yanalenga kufikia dira ya taifa ifikapo mwaka 2025 nchi kuwa ya kipato cha kati.
Mwisho.