Friday, September 13, 2013

Tuko tayari kuimarisha zaidi elimu ya juu nchini — Dkt Kawambwa


Kaimu Mwenyekiti wa jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Prof. Josephat Itika (kushoto) akizungumza na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Dkt. Shukuru Kawambwa aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha jana.  Katikati ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawalana Fedha, Prof. Faustin Kamuzora.


Kaimu Mwenyekiti wa jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Prof. Josephat Itika (kushoto) akimpatia zawadi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Dkt. Shukuru Kawambwa aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha jana.

Na Mwandishi wetu, Arusha
Serikali imesema kwamba iko tayari kutoa ushirikiano zaidi wa mikakati itakayoanzishwa kupanua wigo wa mahusiano kati ya vyuo vya elimu ya juu kwa upande mmoja na waajiri ikiwemo makampuni na viwanda kwa upande mwingine kuongeza thamani ya elimu hapa nchini.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Dkt. Shukuru Kawambwa amesema hayo alipokua akifungua kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha jana.

Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu uliotayarishwa na jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) ni jinsi gani vyuo vikuu vinaweza kushirikiana na waajiri ikiwemo viwanda na makampuni ili kujenga elimu ya juu endelevu Tanzania.

Waziri alisema kuwa serikali kupitia wizara yake itahakikisha inafanyia kazi na kufuatilia mapendekezo yatakayotokana na kongamano hilo la siku mbili.

“Ninataraji kuwa CVCPT na wadau wengine watashirikiana na wizara yangu kuhakikisha mapendekezo ya kongamano hili yanakua yenye manufaa kwa nchi yetu,” alisema.

Alisema wizara yake kupitia programu mbalimbali inazingatia na kutambua umuhimu wa makampuni na viwanda katika kuendeleza elimu.

Alitoa wito kwa CVCPT kuhakikisha inaendeleza makongamano kama haya ili kuifanya elimu nchini kuwa ya thamani na endelevu.

“Ninatoa wito pia kwa wakuu wasaidizi wa vyuo vikuu nchini kuhudhuria kwa wingi katika makongamano mengine siku zijazo,” alisema.

Katibu Mtendaji wa sekretarieti ya Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA), Prof. Mayunga Nkunya alisema kwamba chombo hicho kinaunga mkono ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi.

Alisema IUCEA iko katika mikakati mbalimbali kufanikisha hilo kama kushiriki majadiliano ya kuimarisha mitaala, na kuongeza mahusiano na sekta binafsi katika tafiti na ubunifu.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Prof. Sylvia Temu alisema ushirikiano kati ya vyuo vikuu na waajiri lazima uanzie katika ngazi za juu vyuoni.

“Muda sasa umefika kwa makamu wakuu wa vyuo kutenga muda na kuwa na wadau katika viwanda na makampuni ili kuona jinsi ya kufanya kazi pamoja,” alisema.

Alisema Wizara inaunga mkono ushirika wa aina hiyo maana ndio unaochochea matumizi bora na yenye tija ya utaalamu na elimu.

Kaimu Mwenyekiti wa CVCPT, Prof. Josephat Itika alishukuru wafadhili waliofanikisha kongamano hilo wakiwepo Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Tanzania Investment Bank (TIB) na Tume ya

Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Tunawahakikishia kuwa tutafanyia kazi mchango wao na kuleta ufanisi kama inavyotakiwa,” alisema.

Lengo kubwa la CVCPT ni kukutanisha wadau wa elimu ya juu kwa upande mmoja na wadau wengine wa maendeleo nchini kwa lengo la kujadiliana jinsi ya kuimarisha elimu ya juu na raslimali watu hapa nchini.

CVCPT ilianzishwa mwaka 2005.

Wajumbe wa CVCPT ni makamu wakuu wa vyuo vikuu pamoja na wakuu wa taasisi za elimu binafsi na vya umma pamoja na katibu mtendaji wa TCU.
 Kama mwenyekiti wa sasa wa CVCPT, Chuo kikuu Mzumbe kimekua kikitayarisha kongamano hilo kwa mwaka wa pili mfululizo sasa.

 Mwisho.








Picha kutoka Mkutano wa Matumizi ya Mkongo wa Mawasiliano katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi Afrika Mashariki, Kati na Kusini uliofanyikia Kunduchi beach hotel, Dar es Salaam.


Waziri wa Mawasliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa katikati akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa matumizi ya Mkongo wa Mawasiliano katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, kushoto ni Waziri wa Sayansi na Mawasiliano wa Sudan, Dkt. Eisa Bashari Mohmed Hamid wa Sudan na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA, Profesa John Nkoma, mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi nane.




Waziri wa Mawasliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa (wapili kulia) akichangia mada  wakati wa mkutano wa matumizi ya Mkongo wa Mawasiliano katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini,wapili kushoto ni Waziri wa Sayansi na Mawasiliano wa Sudan, Dkt. Eisa Bashari Mohmed Hamid wa Sudan, Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano nchini (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA, Profesa John Nkoma, mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi nane.

Tuesday, August 27, 2013

TNBC yaishauri Manyara kutumia vyema maazimio ya mkutano wa uwekezaji

Na Mwandishi wetu, Manyara
Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) limewashauri viongozi wa mkoa wa Manyara kuhakikisha kuwa wanatekeleza yale yaliyokubaliwa wakati wa kongamano la maswala ya uwekezaji lililomalizima hivi karibuni kwa faida ya mkoa huo na taifa zima kwa ujumla.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw. Raymond Mbilinyi aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa mkoa huo kupitia baraza la biashara la mkoa linatakiwa kuainisha nini cha kuanza nacho, muhusika na muda maalum wa utekelezaji wa maazimio hayo.
“Kama haya yatafanyika, Manyara itapiga hatua kwa haraka,” alisema na kuongeza kuwa changamoto zilizoainishwa zichukuliwe na kubadilishwa kama fursa.
Alisema mkoa wa Manyara una uwezo wa kufanya vyema katika biashara na uwekezaji na kuwa moja ya vitovu vikubwa vya maendeleo katika ukanda wa kaskazini na nchi kwa ujumla. 
Bw. Mbilinyi alitoa wito kwa mabaraza ya biashara ya mikoa mingine hapa nchini kukaa na kuangalia fursa, changamoto na taarifa nyingine muhimu na kuziwasilisha TNBC kabla ya mikutano ya majadiliano kati ya wawekezaji wa Kitaifa na ule wa Kimataifa kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine mwezi Novemba mwaka huu.
“Rais alishatangaza kufanyika kwa mikutano hii mwezi Novemba…ni vyema mabaraza ya mikoa yakatumia fursa hii vizuri,” alisema.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu alisema wafanyabiashara wa mkoa wa Manyara wajipange na kufanya shughuli zao kwa kufuata kanuni za biashara na kwa weledi.
“Wafanyabiashara ni moja ya wadau wakubwa sana katika kujenga sekta binafsi yenye nguvu,” alisema.
Dkt. Nagu alitoa shukrani kwa taasisi za fedha zilizoshiriki katika mkutano huo wa wawekezaji na kusema kuwa uwekezaji wowote na biashara vinahitaji mitaji ambayo hutolewa na taasisi hizo.
Alisema kuwa mkoa wa Manyara una fursa nyingi ambazo kama zikitumika vyema zitasaidia kuleta maendeleo ya harakana endelevu.
Alitaja baadhi ya vivutio hivyo vya uwekezaji kama hifadhi ya taifa ya Manyara, Tarangire, mlima wa Hanan’g ambao ni wa tatu kwa urefu hapa nchini, ziwa Babati na fursa za kilimo na madini.
Waziri huyo alisema kuwa umefika wakati kwa mkoa wa Manyara na taifa kuanza kufaidika pale kila madini ya aina ya Tanzanite yatakapokua yanauzwa popote duniani kupitia haki inayopatikana chini ya taratibu za kimataifa zinazokubalika.
Alisema nchi ya Ethiopia ilifanikiwa kupitia utaratibu huo na kufaidika na kwamba popote kahawa ya nchi hiyo ilipokua inauzwa popote duniani, sehemu ya faida ilikua inarudi katika nchi hiyo.
“Kama Ethiopia waliweza kwanini sisi tushindwe?,” alisema, na kuongeza kuwa hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya mkoa huo na nchi kwa ujumla.
Mwisho.

Friday, May 24, 2013

Makandarasi nchini watakiwa kuungana




The registrar of Contractors Registration Board (CRB), Eng. Boniface Muhegi addressing participants of the CRB’s annual consultative meeting that started yesterday in Dar es Salaam.
Msajili wa bodi ya makandarasi nchini (CRB), Eng. Boniface Muhegi akihutubia mkutano mkuu wa majadiliano wa bodi hiyo ulioanza jana jijini Dar es Salaam



The registrar of Contractors Registration Board (CRB), Eng. Boniface Muhegi (centre) following up proceedings during the board’s annual consultative meeting that started yesterday in Dar es Salaam.  Others in the picture are the CRB board chairperson, Eng. Consolata Ngimbwa (right) and Tunduru Member of Parliament, Eng. Ram Makani.
Msajili wa bodi ya makandarasi nchini (CRB), Eng. Boniface Muhegi (katikati) akifuatilia jambo wakati wa mkutano mkuu wa majadiliano wa bodi hiyo ulioanza jana jijini Dar es Salaam.  Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa bodi wa CRB, Eng. Consolata Ngimbwa (kulia) na mbunge wa jimbo la Tunduru, Eng. Ram Makani.


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) imetoa wito kwa makandarasi nchini kuhakikisha kuwa wanaungana ili kujenga umoja na nguvu na kupata miradi mikubwa.
Wito huu umetolewa na Mwenyekiti wa bodi ya CRB, Eng. Consolata Ngimbwa alipokua akiongea wakati wa  mkutano mkuu wa mwaka wa  majadiliano wa bodi hiyo ulioanza jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kuungana kutasaida makandarasi wa ndani kuwa na nguvu na pia kuweza kushindana na wale wa nje ambao wengi wao wana nguvu za mitaji, na utaalamu.
“Tuungane ili na sisi tuweze kupata sifa za kupata miradi mikubwa,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema kuwa makandarasi wa madaraja ya juu washirikishe wale wa madaraja ya chini ili waweze kufanya kazi pamoja kwa faida yao wote na kwa faida ya taifa kwa ujumla.
“Makandarasi wa madaraja ya juu waruhusu ushirika na wale wa madaraja ya chini ili kuleta mafanikio zaidi,” alisema.
Akiongea awali, msajili wa Bodi hiyo injinia Boniface Muhegi alisema bodi hiyo imefanikisha mambo mengi tangu kuanzishwa kwake miaka 15 iliyopita.
Alisema kuwa sekta ya ujenzi Tanzania imepiga hatua kubwa kwani kulikuwa na makandarasi wapatao 1000 miaka 15 iliyopita kulinganisha na sasa ambapo kuna jumla ya makandarasi 7000.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuwa na ofisi za kanda katika mikoa minne ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam pamoja na kuongezeka kwa kazi zinazofanywa na makandarasi wazalendo toka asilimia tano mwaka 1998 hadi asilimia 40 leo huku asilimia 60 ya kazi bado zikifanywa na wageni.
“Pia pamekua na ongezeko la ubora na uwingi wa kazi za ukandarasi wa ujenzi,” alisema huku akitolea mfano ongezeko la minara ya mawasiliano ya simu za mkononi ambayo imetapakaa karibu nchi nzima, barabara na majengo ya kisasa.
“Pamoja na vikwazo mbalimbali, tumepiga hatua kubwa,” alisema.
Kwa upande wake, msajili msaidizi, Utafiti na Maendeleo wa bodi hiyo, Eng. Magesa Bairi alisema bodi itaendelea kuwezesha makandarasi nchini kwa njia ya mafunzo na pia kutunisha mfuko wa kusaidia makandarasi hapa nchini.
Eng. Magesa alisema kuwa pamoja na maendeleo hayo kuna changamoto ambazo zinawakabili kama kujenga uwezo wa wakandarasi wazalendo kwa viwango vinavyotakiwa, na pia kutofuata kanuni na sheria mbalimbali kwa upande wa makandarasi.
Mkutano huo wa siku mbili unalenga kuangalia hasa changamoto na mafanikio katika sekta ya ujenzi Tanzania ndani ya miaka kumi na tano iliyopita.
Mapendekezo ya mkutano huo yatapelekwa kwa wadau husika na baadae kufuatilia utekelezaji wake.
Takwimu zinaonyesha kwamba sekta ya ujenzi inachangia asilimia saba ya pato la taifa huku ukuaji wake kwa mwaka ikikadiliwa kuwa ni asilimia kumi na moja ikiwa ni sekta ya pili kwa kasi ya ukuaji huku sekta ya madini ikiongoza.
Asilimia sitini ya bajeti ya maendeleo nchini inakwenda kwenye sekta ya ujenzi huku asilimia themanini ya fedha hizo zikienda kwa wanachama wa bodi ya usajili wa mandarasi wa ujenzi.
Inatarajiwa kuwa kesho Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Pombe Magufuli atazungumza na kushiriki mkutano huo.
Mwisho.