Na Mwandishi wetu, Manyara
Baraza la Biashara la Taifa (TNBC)
limewashauri viongozi wa mkoa wa Manyara kuhakikisha kuwa wanatekeleza yale
yaliyokubaliwa wakati wa kongamano la maswala ya uwekezaji lililomalizima hivi
karibuni kwa faida ya mkoa huo na taifa zima kwa ujumla.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw.
Raymond Mbilinyi aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa
mkoa huo kupitia baraza la biashara la mkoa linatakiwa kuainisha nini cha
kuanza nacho, muhusika na muda maalum wa utekelezaji wa maazimio hayo.
“Kama haya yatafanyika, Manyara
itapiga hatua kwa haraka,” alisema na kuongeza kuwa changamoto zilizoainishwa
zichukuliwe na kubadilishwa kama fursa.
Alisema mkoa wa Manyara una uwezo wa
kufanya vyema katika biashara na uwekezaji na kuwa moja ya vitovu vikubwa vya
maendeleo katika ukanda wa kaskazini na nchi kwa ujumla.
Bw. Mbilinyi alitoa wito kwa mabaraza
ya biashara ya mikoa mingine hapa nchini kukaa na kuangalia fursa, changamoto
na taarifa nyingine muhimu na kuziwasilisha TNBC kabla ya mikutano ya
majadiliano kati ya wawekezaji wa Kitaifa na ule wa Kimataifa kwa upande mmoja
na serikali kwa upande mwingine mwezi Novemba mwaka huu.
“Rais alishatangaza kufanyika kwa
mikutano hii mwezi Novemba…ni vyema mabaraza ya mikoa yakatumia fursa hii
vizuri,” alisema.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu alisema wafanyabiashara wa
mkoa wa Manyara wajipange na kufanya shughuli zao kwa kufuata kanuni za
biashara na kwa weledi.
“Wafanyabiashara ni moja ya wadau
wakubwa sana katika kujenga sekta binafsi yenye nguvu,” alisema.
Dkt. Nagu alitoa shukrani kwa taasisi
za fedha zilizoshiriki katika mkutano huo wa wawekezaji na kusema kuwa
uwekezaji wowote na biashara vinahitaji mitaji ambayo hutolewa na taasisi hizo.
Alisema kuwa mkoa wa Manyara una
fursa nyingi ambazo kama zikitumika vyema zitasaidia kuleta maendeleo ya
harakana endelevu.
Alitaja baadhi ya vivutio hivyo vya
uwekezaji kama hifadhi ya taifa ya Manyara, Tarangire, mlima wa Hanan’g ambao
ni wa tatu kwa urefu hapa nchini, ziwa Babati na fursa za kilimo na madini.
Waziri huyo alisema kuwa umefika
wakati kwa mkoa wa Manyara na taifa kuanza kufaidika pale kila madini ya aina
ya Tanzanite yatakapokua yanauzwa popote duniani kupitia haki inayopatikana
chini ya taratibu za kimataifa zinazokubalika.
Alisema nchi ya Ethiopia ilifanikiwa
kupitia utaratibu huo na kufaidika na kwamba popote kahawa ya nchi hiyo
ilipokua inauzwa popote duniani, sehemu ya faida ilikua inarudi katika nchi
hiyo.
“Kama Ethiopia waliweza kwanini sisi
tushindwe?,” alisema, na kuongeza kuwa hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya
mkoa huo na nchi kwa ujumla.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment