Thursday, March 26, 2015

Huduma TPA kuimarika kufuatia kujiunga na mkongo wa mawasiliano

Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Killiani Chale (kushoto) akipokea cheti cha Mamlaka hiyo kuunganishwa na mkongo wa mawasiliano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ambapo matawi 13 ya mamlaka hiyo yameunganishwa na mfumo huo wa mawasiliano.  Hafla hiyo iliambatana na mamlaka hiyo kukabidhiwa mradi huo baada ya kukamilika.  Kulia ni Ofisa Mkuu wa Ufundi wa TTCL, Bw. Senzige Kisenge.  Tukio hilo lilifanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) zinatarajiwa kuimarika kufuatia hatua ya makao makuu ya mamlaka hiyo kuunganishwa kupitia teknolojia ya kisasa na matawi yake 13 nchini.

Mradi huo uliokwishaanza kutekelezwa unafuatia kuunganishwa kwa TPA na mkongo wa mawasiliano wa Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) kupitia mfumo unaoitwa Multiprotocal Label Switching Virtual Private Network (MPLS VPN).
Kupitia mfumo huo wa MPLS VPN, huduma za sauti, data na intaneti za TPA zinatarajiwa kuimarika kwa kiwango kikubwa.

“Mradi huu uliotekelezwa na TTCL utatusaidia kuimarisha huduma za bandari zetu pamoja na wateja wetu,” Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa TPA, Bw. Killian Chale alisema wakati wa kukabidhiwa rasmi mradi huo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Matawi ya TPA yaliyounganishwa na mfumo huo wa mawasiliano ni pamoja na ofisi ya makao makuu TPA, bandari za Mwanza, Kigoma, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam, Mafia, Lindi, Kilwa, Pemba, Bukoba, Nansio na Musoma.


Kwa mujibu wa Bw. Chale, sasa mawasiliano kati ya bandari moja na nyingine yatatumia mfumo wa CISCO ambao ni wa gharama nafuu na usikivu wake ni bora zaidi.

No comments: