Katibu Mtendaji wa Baraza
la Taifa la Biashara (TNBC) Mhandisi Raymond Mbilinyi (kulia) akibadilishana
mawazo na Mkurugenzi wa Global Industrial Park Ltd, Bw. Zainuddin Adamjee
muda mfupi mara baada ya kumaliza kwa kikao cha baraza la biashara la mkoa wa
pwani hivi karibu mjini Bagamoyo. Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau toka
sekta ya umma na binafsi.
Na Mwandishi
Wetu, Bagamoyo
Baraza la
Biashara la mkoa wa Pwani limetakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
wawekezaji waliowekeza katika maeneo maalumu ya ukanda wa uwekezaji mkoani
humo.
Katibu Mtendaji
wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Mhandisi Raymond Mbilinyi amesema hivi
karibuni mkoani hapa kuwa maeneo maalum ya ukanda ya uwekezaji ni njia bora ya
kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama yataendelea kwa kiwango
kinachotakiwa.
“Nchi nyingi
zimefikia maendeleo kwa kutumia njia hii ya kuwekeza katika maeneo maalum, kama
baraza la mkoa ni muhimu mkahakikisha yanaendelea bila tatizo,” alisema.
Akiongea katika
kikao cha baraza la mkoa huo hivi karibuni mjini Bagamoyo, alisema ukanda huo
maalumu katika mji huo utasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa ajira pamoja
na kuinua kipato cha wakazi wa mji huo.
“Sasa hivi kuna tatizo
la ajira katika miji yetu, hivyo uwepo wa viwanda utasaidia vijana wengi kupata
ajira,” aliongeza.