Wednesday, January 21, 2015

Serikali yapewa changamoto kuchochea ubunifu kwa wanafunzi



Na Mwandishi wetu, Morogoro

Serikali imeshauriwa ipitie upya mitaala yake ya  elimu ili iweze kuendana na ulimwengu wa utandawazi ambao unafanya mwanafunzi kuwa mbunifu zaidi.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Ndetembia Matemu, Bw. Joshua Kihaka amesema mjini Morogoro hivi karibuni kuwa mitaala ya elimu inatakiwa kuangaliwa upya ili iende sambamba na wakati.

“Wanafunzi wanatakiwa kupata maarifa yatakayowafanya kuwa wabunifu,” alisema.

Alisema pamoja na changamoto hiyo shule ya Ndetembia Matemu inawandaa wanafunzi wakubalike kitaifa na kimataifa kulingana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Alifafanua kuwa shule hiyo inayofundisha kwa lugha ya kiingereza pia inafundisha somo la Teknolojia ya Habari na Mawaslianino (TEHAMA) ambalo linawafanya watoto kwenda na wakati.

Alisema changamoto za kielimu zilizopo nchini lazima zitatuliwe na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, walimu na wazazi.

Serengeti Ltd yawaahidi makubwa wakulima wa shayiri nchini



Na Mwandishi wetu, Siha

Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) imesema kwamba wakulima katika kanda za kilimo cha shayiri Tanzania wategemee ushirikiano zaidi kupitia mpango wa kampuni hiyo kushirikiana na wakulima wadogo wa zao hilo nchini.

Akiongea na waandishi wa habari wilayani Siha mkoa wa Kilimanjaro hivi karibuni, Meneja Kilimo Biashara wa kampuni hiyo ya SBL, Bw. Shafii Mndeme alisema mkakati huo uko mbioni kuimarishwa katika miaka miwili ijayo na zaidi.

Kwa mujibu wa mpango huo, kampuni hiyo inawasaidia wakulima wa shayiri mbegu na kuwaunganisha na wataalamu wengine wa kilimo ambapo hatimae hununua zao hilo.

Kampuni hiyo pia inasaidia wakulima kupata elimu kuhakikisha kuwa mazao wanayozalisha yanakua ya kiwango bora kwa uzalishaji wa bia pamoja na kuongeza uzalishaji kwa heka.

“Wakulima wa shayiri nchini walime zao hilo maana mpango huu unazidi kukua siku hadi siku,” alisema mara baada ya kugawa mbegu za zao hilo kwa wakulima wa kijiji cha Ngare Nairobi wilayani Siha.

DART yachukuliwa kupunguza msongamano kituo cha Ubungo



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Hatua kadhaa zimechukuliwa kujaribu kurahisisha utokaji wa mabasi ya kwenda mikoani katika kituo cha mabasi cha Ubungo (UBT).

Hatua hizo, zilizokubaliwa jana na wakala wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART),mshauri wa mradi wa DART, SMEC na mkandarasi wa mradi huo, STRABAG zinalenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo hasa nyakati za asubuhi, mabasi hayo yanapokuwa yanatoka kuelekea mikoani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa miundombino na Uendeshaji wa wakala wa DART,Mhandisi John Shauri, ukingo unaotazamana na Geti namba 1 la Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) unaotenga barabara ya kawaida na njia ya mradi utabaki kama ulivyojengwa.

Mhandisi aliongeza kuwa mabasi ya mikoani yanayoondoka UBT kupitia Geti namba 1 au 2 yataruhusiwa kutumia njia za mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) zinazotazamana na Geti namba 2 na kisha kugeuza kwa kutumia njia hizo wanapofika katika kituo cha basi cha mradi cha BRT Ubungo na kuelekea katika mataa ya Ubungo yakitumia njia hizo hizo za mradi.

“Baada ya hapo watatumia barabara ya kawaida kuelekea Kimara,” ilisema na kuongeza kuongeza mabasi hayo yatatumia kwa muda kwenye njia hizo mpaka pale tu huduma za kipindi cha mpito (interim service) kwenye barabara za mfumo wa mabasi yaendayo haraka kitapoanza.

Thursday, January 15, 2015

Wakulima Manyara, K’njaro wasifu ushirikiano na Serengeti Ltd

Meneja Kilimo Biashara wa kampuni ya bia ya Serengeti (SBL), Bw. Shafii Mndeme (wa pili kulia) akimkabidhi mbegu za shayiri mkulima Norbert Malihela wa kata ya Basutu, wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara hivi karibuni. Maafisa wa kampuni hiyo walifanya zoezi la kukabidhi mbegu hizo kwa wakulima wa mikoa ya Manyara na Kilimanjaro chini ya mpango wa ushirikiano kati ya kampuni hiyo na wakulima wa shayiri nchini. Wengine ni Bw. Dominick Daniel (kulia) na Bw. Mwinyi Makame (mwenye miwani), wakulima wa shayiri katika kata hiyo.
Meneja Kilimo Biashara wa kampuni ya bia ya Serengeti (SBL), Bw. Shafii Mndeme (kulia) akimkabidhi mbegu za shayiri mkulima Mwinyi Makame wa kata ya Basutu, wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara hivi karibuni. Maafisa wa kampuni hiyo walifanya zoezi la kukabidhi mbegu hizo kwa wakulima wa mikoa ya Manyara na Kilimanjaro chini ya mpango wa ushirikiano kati ya kampuni hiyo na wakulima wa shayiri nchini. Kushoto mwenye miwani ni Afisa Ugani wa kampuni ya SBL, Bw. Peter Ndilahomba.
Na Mwandishi wetu, Manyara

Wakulima wa shayiri katika mikoa ya Manyara na Kilimanjaro wamesifu mpango wa ushirikiano kati ya kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) na wakulima wadogo nchini na kusema kuwa umeongeza thamani ya kazi yao.

Wakizungumza katika nyakati tofauti wakati wa kupokea mbegu za shayiri kutoka SBL hivi karibuni, wakulima hao wamesema ushirikiano huo hauna budi kuimarishwa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa mujibu wa mpango huo, kampuni hiyo inawasaidia wakulima wa shayiri mbegu na kuwaunganisha na wataalamu wengine wa kilimo ambapo hatimae hununua zao hilo.

Kampuni hiyo pia inasaidia wakulima kupata elimu kuhakikisha kuwa mazao wanayozalisha yanakua ya kiwango bora kwa uzalishaji wa bia pamoja na kuongeza uzalishaji kwa heka.

Mkulima wa shayiri katika kata ya Basutu wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Bw. Nobert Malihela alisema mpango huo wa ushirikiano umesaidia wakulima katika kata hiyo kupata mbegu kwa wakati na hivyo kupanda kwa wakati.


“Tunapata mbegu kwa wakati na hii inatuwezesha kupanda katika muda unaotakiwa na kupata mazao ya kuridhisha,” alisema na kuongeza kuwa mpango huo hauna budi kusambazwa kwa wakulima zaidi hapa nchini.