Na Mwandishi wetu, Dar
es Salaam
Serikali ya Tanzania
imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na wadau
wengine ili kufikia mapinduzi ya kilimo hapa nchini na hivyo kupatikana usalama
wa chakula na maendeleo.
Msimamo huo umetolewa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akifungua mkutano mkubwa wa kilimo
unaofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo wa siku
mbili umetayarishwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa kushirikiana na
Ofisi ya Waziri Mkuu na Kituo cha mpango maalum wa uendelezaji kilimo katika
ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Mkutano huo unalenga
kuvutia wawekezaji katika maeneo ya kilimo, biashara na miradi ya maendeleo
kijamii na kiuchumi katika eneo la SAGCOT.
“Ushirikiano uliopo
kati ya serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, wakulima na wadau wengine
wa kilimo umesaidia kuendeleza sekta hii hapa nchini,” alisema.
Waziri Mkuu
aliyashukuru makampuni 20 ambayo tayari yameshatoa ahadi ya kuwekeza katika
sekta ya kilimo Tanzania katika miaka ijayo na wakati huo huo akaitaka sekta
binafsi kufanya uamuzi zaidi wa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo.
Hata hivyo alisisitiza
kwamba wawekezaji wote katika ukanda wa SAGCOT watapewa kipaumbele pale ambapo
uwekezaji wao unalenga pia kushirikisha wakulima wadogowadogo..
“Ni muhimu kusisitiza
kwamba tunahitaji zaidi uwekezaji ambao utajali kushirikiana na wakulima wadogo
na wajasiriamali wadogo na wa kati,” alisema.
Alisisitiza kwamba hata
mapendekezo ya sera za uwekezaji katika kilimo zitoe kipaumbele kueleza jinsi
wakulima wadogo na watanzania wa kawaida watakavyofaidika na uwekezaji katika
ukanda wa SAGCOT.
Waziri Mkuu
aliwahakikishia wawekezaji kwamba kupitia sheria mbalimbali Tanzania inatoa
vivutio vingi na vizuri kulinganisha na nchi nyingine za Afrika.
“Kuwekeza Tanzania pia
kunawahakikishia soko la uhakika katika eneo hili la Afrika,” alisema.
Alisema Tanzania
imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohakikisha usalama wa wawekezaji.
Akitoa mada katika
mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza
alitaja baadhi ya maeneo yanayolengwa katika uwekezaji SAGCOT kama kilimo cha
miwa, matunda, ufugaji, nafaka na mazao ya misitu.
Katika siku ya pili ya
mkutano huo wawekezaji watapata fursa ya kutembelea maeneo maalum ya miradi
pamoja na kuangalia miradi ya kuimarisha miundombinu katika ukanda huo wa
SAGCOT.
SAGCOT ni mpango
unaoshirikisha sekta binafsi na ya umma unaotegemewa kuleta mapinduzi makubwa
katika usalama wa chakula nchini kwa kushirikisha pia wakulima wadogo wadogo
katika mazingira endelevu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment