Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA)
imesaini makubaliano na Water Resources Corporation (K Water) ya Korea Kusini
kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa uzalishaji wa nishati ya umeme na maji kwa
matumizi mbalimbali katika Bonde la Mto Ruaha mdogo.
“Tumekuatana hapa leo kufikia makubaliano na wenzetu wa
Kampuni hii ya Korea Kusini kuanza kufanya upembuzi yakinifu wa kuzalisha
nishati ya umeme, kupata maji kwa ajili ya Manispaa ya Iringa na maji kwa ajili
ya kilimo cha umwagiliaji kwa wananchi wa maeneo hayo,”alisema Mkurugenzi Mkuu
wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam.
Alisema Mkoa wa Iringa umepata bahati ya kuwa na mvua za
kutosha na kwamba mto huo unaweza kuwa chanzo kizuri cha kuzalisha umeme,
matumizi bora ya maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kwa ajili ya kilimo
cha umwagiliaji.
Maeneo ambayo yana uwezekano wa kuzalisha umeme katika bonde
hilo ni pamoja na maanguko ya Tosamaganga, Manyandamonda, Ibosana Nginayo.
Alisema kampuni hiyo itafanya kazi hiyo kwa kipindi cha mwaka
mmoja ili kuona kama kuna uwezekano wa kupata huduma zote za umeme, matumizi ya
kawaida na umwagiliaji au kupata mojawapo.
Alisema mwaka 1984 Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Norway NORAD lilifanya upembuzi yakinifu katika eneo hilo na kubaini kuwa linauwezo
wa kuzalisha Megawati 87.
“Umeshapita muda mrefu, sasa tunataka kuangalia kama bado
uwezo ni huo la mambo yamebadilika,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi RUBADA, Profesa Raphael
Mwalyosi alisema mto Ruaha mdogo una maji kwa kipindi chote cha mwaka kutokana
na mazingira mazuri ya mvua za kutosha.
“Tukifanikiwa katika hili itakua ni kichocheo kikubwa cha maendeleo
kwa sababu Iringa inakua kwa kasi, kuna viwanda na huduma za maji zinahitajika,”alisema
Profesa Mwalyosi.
Alisema maji hayo yanaweza kutumika katika matumizi mseto ikiwa
ni pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, kilimo, mifugo na matumizi ya watu na hivyo
kuwa chachu ya maendeleo.
Alisema ni muhimu kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa ili
kuwa ma matumizi yanayoendana na mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya kuwa na
mazingira endelevu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Water Resources
Corporation ya Korea Kusini, Bw. Woo Kyu, Kang alisema kampuni yao ni kongwe na
yenye uzoefu mkubwa.
Ilianzishwa mwaka 1967 na imejihusisha na miradi mikubwa ya
uzalishaji umeme ikiwemo ya nchini Philipines na Pakistan.
Alisema mradi wa Iringa katika Bara la Afrika wanauchukulia
umuhimu mkubwa kwa faida ya pande zote mbili.
“Tunashukuru kwa serikali ya Tanzania kuonyesha uaminifu
kwetu,” alisema.
Alisema wanategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau
mbalimbali hapa nchini ili kukamilisha kazi watakayoanza kufanya na kuahidi
kuifanya kwa uaminifu na ufanisi mkubwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment