Tuesday, September 18, 2012

Serikali yahakikishia vyuo vikuu ushirikiano zaidi


Na Mwandishi wetu, Arusha

Serikali imehakikishia taasisi za elimu ya juu hapa nchini kuwa itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kisera na kuhakikisha kuwa elimu inaendelea kuwa chachu kubwa kufikia malengo ya maendeleo ya nchi ya 2025.

Haya yamesemwa na waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa wakati wa kongamano la nne la Elimu ya Juu jana jijini Arusha.

Kongamano hilo linaloisha leo limetayarishwa na kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Wakuu wa Vyuo nchini Tanzania (CVCPT) kwa kushirikiana na taasisi ya Trust Africa.

Kauli mbiu ya Kongamano hili ni Utawala Bora kwa Elimu Bora Endelevu ya Vyuo Vikuu Tanzania.

“Hakuna nchi inayoweza kujipatia maendeleo makubwa bila kuwa na idadi ya kutosha ya wasomi katika nyanja mbalimbali,” alisema Dkt. Kawambwa ambae alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo.

Alisema ili mahitaji ya raslimali watu na malengo ya maendeleo ya kitaifa ifikapo mwaka 2025, nchi haina budi kuzalisha walau wahitimu 80,000 toka katika vyuo vikuu.

Alisema kwa juhudi za serikali imewezekana kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kwa asilimia 19 kutoka wanafunzi 139,638 mwaka 2010/2011 hadi 166,484 mwaka 2011/2012.

“Hii imetokana pamoja na mambo mengine kwa sababu ya ongezeko la vyuo kufikia 46 hapa nchini,” alisema.

Alisema kutekeleza utawala bora ni changamoto, lakini swala hilo lazima lifanyike kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Ni lazima utawala bora utekelezwe katika vyuo vikuu, sio kwa maneno tu, bali kwa vitendo,” alisema.

Mwenyekiti wa CVCPT Prof. Joseph Kuzilwa alisema majadiliano ya kongamano hilo yataletelea maazimio yanayofaa ya kisera katika kuendesha vyuo vikuu nchini na hivyo kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi.

Chuo Kikuu Mzumbe kama Mwenyekiti wa sasa wa CVCPT, kimepewa jukumu kwa niaba ya CVCPT kuwa mwandaaji wa kongamano hili.

Kwa mujibu wa Prof. Kuzilwa malengo ya kongamano hilo ni kutathmini ubora wa mifumo ya utawala na kuangalia ni kwa kiasi gani inakwamisha utawala bora katika vyuo vikuu, kuangalia changamoto zinazovikabili vyuo vikuu na namna gani utawala bora unaweza kutua changamoto hizo na kuanzisha mikakati ya pamoja kwa ajili ya kuimarisha utawala bora katika vyuo vikuu.

Mada zinazowasilishwa ni pamoja na utawala na utendaji kazi wa Vyuo Vikuu nchini Tanzania : Hali halisi na Changamoto;  ufadhili wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu;  mifumo ya utawala, michakato, mahusiano na fursa za kuendesha vyuo vikuu;  na serikali za wanafunzi na demokrasia katika vyuo vikuu.

Mada nyingine ni nafasi ya teknolojia, habari na mawasiliano (TEHAMA) katika utawala wa vyuo vikuu nchini Tanzania; utawala, kujitawala na ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania na taratibu za ugawaji kazi na menejimenti ya raslimali watu katika Vyuo Vikuu nchini Tanzania: Tunajifunza nini kutoka kwa kila mmoja wetu.

CVCPT imeanzishwa chini ya kifungu cha 53 cha Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005.

Wanachama wa CVCPT ni Makamu Wakuu wa Vyuo, Wakuu wa Vyuo kutoka Vyuo Vikuu vya umma na binafsi hapa nchini pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU). Jukumu kubwa la kamati hii ni kuishauri TCU na serikali kwa ujumla kuhusiana na masuala ya wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini.

Mwisho 

No comments: