Tuesday, September 18, 2012

Mradi wa Makaa ya Mawe Ngaka kupunguza ghrama za uzalishaji viwandani


Na Mwandishi wetu, Mbinga
 Uzalishaji katika viwanda nchini unatarajia kuimarika zaidi kutokana na mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka, makaa hayo mengi na bora zaidi katika Mkoa Ruvuma ,Wilaya ya Mbinga katika kijiji cha Ruanda yanapatikana kwa gharama nafuu ambapo itasaidia kutoa msukumo mkubwa katika uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa Kampuni ya TANCOAL,Bw.Graeme Robertson alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kujionea maendeleo ya mradi huo wa makaa ya mawe na gesi asilia ambayo imegundulika katika eneo la mradi wa Makaa ya mawe Ngaka ambapo katika ziara hiyo aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC),Bw.Gideon Nasari na Mbunge wa Mbinga Mashariki Bw.Gaudence Kayombo. 
“Mradi huu mkubwa wa taifa umekuja  wakati mwafaka kwa ajili ya kupata nishati kwa gharama nafuu kwa ajili ya viwanda vyetu kwa vile gharama za uzalishaji imekuwa juu kutokana na bei ya nishati ya umeme waoutumia hivi sasa zimepanda,”alisema Bw.Robertson mwishoni mwa wiki.
Alisema mradi huo kuzalisha makaa ya mawe na kuyasambaza kwa watumiaji kwajili ya nishati ya viwandani ambayo inatumika badala ya umeme wa gesi asilia inayotoka mikoa ya kusini na ule wa kufua kupitia mafuta ya dizeli.
“Mbali ya uzalishaji huu wa makaa yam awe tunnajiandaa kujenga  mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 200  ifikapo mwaka 2015,” alisema Bw. Robertson,  ambapo Songea mjini na vijijini pamoja na vijiji vya jirani vilivyopo karibu na eneo la mgodi kuweza kupata nishati ya umeme.
Alisema pia katika mradi wa Ngaka imetokea bahati kubwa ya kugundulika kwa gesi asilia mpya inayokaa chini ya makaa ya mawe ( coal bed methane) ambapo kampuni yao inafanya kazi kwa karibu sana na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) katika kuhakikisha inazalishwa kwa ajili ya watanzania na uchumi wao.
Mbunge wa Mbinga Mashariki, Bw.Gaudence Kayombo alisema mradi wa makaa ya mawe Ngaka unatarajia kukidhi mahitaji ya shida ya nishati ya umeme ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya wakazi wa jimbo lake na Mkoa Mzima wa Ruvuna.
“Ninayo furaha kuwa tangu maradi uanzishwe mwaka 2006 unaendelea vizuri na kwa bahati nzuri eneo hilo pia limegundulika kuwa na gesi asilia chini ya makaa ya mawe ambapo matumaini yetu utaleta kichocheo cha maendeleo kwenye vijiji vyetu vyote kwa kupata umeme,”
Alisema mradi hadi sasa umeleta faida kubwa kwa wananchi hasa vijana wameweza kujipatia ajira na wengine kujiajiri kutokana na kuwepo kwa mradi huo jambo linalochochea kuwepo kwa mzunguko mzuri wa uchumi na maendeleo katika eneo hilo.
Alisema Tanzania pamoja na kwamba kuna sera nzuri, sasa hivi inahitajika kujitayarisha kuona miradi kama hiyo, taifa linakuwa na hisa aslimia 50 na mwekezaji 50 au 49 kwa 51 ili kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kuchota ujuzi na teknoloji mpya.
Alisema pia nchi inatakiwa kujitayarisha mapema kuanza kuandaa kujenga uwezo wa kimtaji na ujuzi ili miradi kama hiyo iweze kufanywa na watanzania wenyewe na wageni wawe wajiriwa tu kwa lengo la kuleta manufaa zaidi kwa nchi.
Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Bw. Gideon Nasari alisema shirika limefanikiwa kufungua mradi wa kwanza wa makaa ya mawe wa Ngaka ambao una mawe mengi na bora zaidi.
“Viwanda vingi hapa nchini sasa vinapata mawe kutoka hapa badala ya Afrika Kusini ambako walikuwa wananunua tani moja dola 250 lakini hapa wananunua nusu ya gharama hiyo hivyo ni neema kwa viwanda vyetu,”alisema Bw.Nasari.
Alisema Pia makaa ya mawe hayo wanauza nchi jirani ya Malawi ambao wananunua kwa ajili ya kukaushia zao la chai na sasa hivi wanajipanga kwaajili ya kuzalisha nishati ya umeme.
Alisema mazungumzo ya makubaliano na TANESCO ya mradi huo kuzalisha umeme yanaendelea ambapo tayari wameshafanya upembuzi yakinifu na tafiti hivyo wanatarajia baada ya kukamirika makubaliano watatafuta vyanzo vya fedha kwa jili ya kujenga mtambo kuzalisha nishati hiyo.
Viongozi hao wa kampuni hiyo ya TANCOAL, Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Mbunge wa Mbinga Mashariki walifanya ziara ya kujionea maendeleo ya mardi na pia kuangalia rasirimali ya gesi asilia ambayo imegundulika katika eneo hilo la mradi.
Mwisho.

No comments: