Friday, September 21, 2012

Maadili ni muhimu kufanikisha TEHAMA vyuo vikuu


Na mwandishi wetu, Arusha
Taasisi za elimu ya juu nchini zimepewa changamoto ya kuzingatia maswala ya maadili katika sera zinazohusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)kama vinataka kupata faida kubwa katika eneo hilo.
Ushauri huu umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT), Taaluma, Fr. Dkt. Thadeus Mkamwa wakati wa kongamano la nne la Elimu ya Juu lililomalizika hivi karibuni jijini Arusha.

“Ni muhimu kuzingatia maswala haya ya maadili katika sera zinazohusu TEHAMA katika taasisi hizi za elimu ya juu…bila kufanya hivi tunaweza kujikuta tumepoteza mwelekeo,” alisema Dkt. Mkamwa, akiongeza kuwa ingawa TEHAMA inafaida kubwa bado pia inaweza kuleta hasara kama maadili katika matumizi yake hayatazingatiwa.

Alisema swala hili ni muhimu zaidi sasa ambapo vyuo vikuu vinakabiliwa na changamoto nyingi, mpya na kubwa.

“Ni vyema tukajua kwamba sasa tuna aina mpya ya wanafunzi ambao wanatumia vifaa vya kisasa kama simu na kompyuta na wamezungukwa na maswala mengi yanayohusu TEHAMA…kama tusipokua makini tutashindwa kuwapatia muongozo unaofaa,” alisema, na kuongeza kwamba vyuo vinatakiwa kuwaongoza wanafunzi kuwa watu gani baadae, wafahamu nini na wafanye nini.
Kwa msingi huo, Dkt. Mkamwa alisema kwamba ni muhimu kuangalia vitu vitakavyosaidia kujua uzuri wa TEHAMA hasa wakati huu ambapo wanafunzi wengi na watu wengi katika familia wanapendelea zaidi kutumia vifaa vya TEHAMA ili kuepuka athari mbaya zinazoweza kutokea na kuondoa faida.
Alisema chuo cha SAUT tayari kinaliangalia hili kwa kufundisha masomo yanayohusiana na maadili ili kuwafanya wanafunzi kujua uzuri na ubaya wa TEHAMA kama isipotumiwa vyema.
“Mtaala wetu unatayarisha wanafunzi kuwa wataalamu na vilevile watu wenye maadili yanayofaa,” alisema.
Mapema, akiwasilisha mada kuhusiana na nafasi ya TEHAMA katika uongozi wa vyuo Tanzania, Prof. Beda Mutagahywa toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema nafasi ya teknolojia katika vyuo vikuu ni swala lisiloepukika.
“Ni lazima taasisi za elimu ya juu ziingize TEHAMA katika mikakati yake na program zake za masomo,” alisema Prof. Mutagahywa.
Alisema ni muhimu vyuo vikuu vikaeleza wazi jinsi teknolojia itakavyosaidia kuimarisha tafiti na vilevile vijenge uwezo katika eneo hilo.

Kauli mbiu katika kongamano hilo lililotayarishwa na kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Wakuu wa Vyuo nchini Tanzania (CVCPT) kwa kushirikiana na taasisi ya Trust Africa ilikuwa
ni Utawala Bora kwa Elimu Bora Endelevu ya Vyuo Vikuu Tanzania.

Washiriki wa kongamano hilo la siku mbili walikuwa pamoja na wenyeviti wa mabaraza ya vyuo vikuu, makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu, Wakuu wa Vyuo, Manaibu wakuu wa Vyuo wa vyuo vyote vya serikali na vya umma, Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na wadau wengine wa elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi.
CVCPT imeanzishwa chini ya kifungu cha 53 cha Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005.

Mwisho

No comments: