Thursday, October 10, 2013

Wekezeni katika maeneo maalumu ya EPZA - Dkt. Kigoda

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Adallah Kigoda akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha Kishen Import and Export Limited jana jijini Dar es salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Bw. Gregory Teo; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa kampuni ya Kishen Import and Export Limited, Bw. Rajen V.Solanki.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Adallah Kigoda (katikati) akisikiliza kwa makini maelezo ya namna ya utengezaji wa pikipiki kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Kishen Import and Export Limited, Bw. Rajen V.Solanki (kushoto) wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) Dkt. Adelhelm Meru.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuzidi kuvutia wawekezaji zaidi ili kuifanya nchi kuingia katika uchumi wa viwanda.
Waziri Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda alisema hayo wakati akizidua Kiwanda cha Kishen Import & Export LTD cha jijini Dae es Salaam jana, kuwa mazingira bora ya uwekezaji ni moja ya vigezo muhimu vinavyosaidia nchi kuingia katika uchunmi wa viwanda.
Kiwanda hicho kilichowekeza chini ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kinatengeneza pikipiki aina ya Toyo za miguu mitatu na miwili.
“Hii ni hatua nzuri na muhimu katika kujenga uchumi wetu,” alisema.
Alisema serikali inajitahidi na imedhamiria kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili taifa liweze kupanua uchumi wake na kutoa ajira kwa watanzania.
Alisema kampuni hiyo ni ya watanzania ambao wamewekeza katika sekta ya viwanda na wanatumia malighafi inayopatikana hapa nchini kwa asilimia 40 na asilimia 60 wapata nje ya nchi.
Alisema watanzania wanatakiwa kuiga mfano huo na kutumia fursa zinazojitokeza na kuwekeza katika maaneo maalumu ya uwekezaji ya EPZA ili washiriki kujenga uchumi wa viwanda.
“Serikali imetengeneza mifumo ya kusaidia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza na kupata mafanikio...wajitokeze na kutumia fursa hizo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru alisema kiwanda hicho kilianzishwa baada ya kupata leseni ya mamlaka yake  na kimeanza kufanya kazi nzuri ya uzalishaji.
“Kiwanda hiki ni moja ya viwanda zaidi ya 70 vilivyo chini ya mamlaka ya EPZA na kinazalisha bidhaa mbalimbali kukidhi mahitaji ya watanzania,” alisema.
Aliongeza kusema viwanda vyote vilivyofanya uwekezaji chini ya EZPA vimewekeza mtaji wa zaidi ya dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 1.15 na kutoa ajira za moja kwa moja  kwa Watanzania 26, 381.
“Haya ni mafanikio makubwa  katika dhana nzima ya kukuza viwanda hapa nchini  na ni matokeo ya azma ya serikali ya kuvutia wawekezaji kujenga uchumi wa kati ifikapo 2025,” alisema.
Alisema EPZA imetenga maeneo ya uwekezaji katika mikoa 20 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na sasa nguvu imeelekezwa zaidi katika maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bagamoyo, Mtwara, Kigoma na Dar es Salaam.
Alisema wawekezaji wanatakiwa kuchangamikia maeneo hayo kujenga viwanda ili bidhaa mbalimbali zizalishwe hapa nchini na kupataikana kwa gharama nafuu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw.Rajen V Solank alisema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2012  kutoka kiwanda dada cha Kishen Enterprises Ltd na kinamilikiwa na watanzania kwa asilimia 100.
“Bidhaa zetu ni kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi,” alisema.
Alisema kiwanda hicho kimewekeza dola za kimarekani milioni 3 na kinazalisha pikipiki 300 kwa mwezi na kimeajiri wafanyakazi 270 kati yao 250 ni watanzania.
Alisema pikipiki za miguu mitatu zinapatikana kwa gharama nafuu na zina uwezo wa kubeba zaidi ya tani moja na kutumika kama gari la wagonjwa na shughuli nyingine za uchumi.
Mwisho  


Monday, October 7, 2013

Kituo cha kibiashara Kurasini chachu kwa uchumi —Dkt. Meru

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt Adelhelm Meru akisisitiza jambo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imesema ujenzi wa kituo kikubwa cha kibiashara kinachotarajiwa kujengwa Kurasini jijini Dar es Salaam kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni kutoka China kitakuwa na manufaa makubwa kiuchumi na ustawi wa jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa maendeleo ya uendelezaji eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha biashara umefikia hatua nzuri.
“Kituo hiki kinajengwa kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania kupitia EPZA na Kampuni hiyo ya ubia kutoka jimbo ya Yig China,”alisema.
Alisema katika kituo hicho kitakuwa na wafanyabiashara mbalimbali pia viwanda vitajengwa na kitawezesha kutoa ajira  zaidi ya 25,000 kwa watanzania kitakapokamilika.
Pia kitawezesha bidhaa za mataifa mbalimbali kupatikana na kupunguza gharama kwa watanzania kwenda nje ya nchi kutafuta bidhaa hizo.
“Serikali itaongeza wigo wa mapato yake kutokana na uwekezaji mkubwa utakaofanyika katika kituo hicho,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa ujenzi unatarajia kuanza baada ya kukamilisha kufanya tathimini na ulipaji fidia makazi ya watu 1012 yaliyopo katika maeneo hayo.
Alifafanua zaidi kuwa ulipaji fidia huo ulio katika awamu tatu utakapokamilika tu ujenzi wa kituo hicho utaanza mara moja.
Awamu ya kwanza ya ulipaji fidia imeanza kutekelezwa ambapo watu 270 tayari wamefanyiwa tathimini na kulipwa na kuongeza kuwa wamepatiwa miezi miwili kuhama maeneo hayo.
Alisema kwa bahati nzuri baadhi ya wananchi wameelewa umuhimu wa ujenzi wa kituo hicho kwa ajili ya maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla.
“Wananchi wanastahili pongezi kwa kukubali fidia na tayari baadhi yao wameanza kuhama kabla ya muda wa miezi miwili waliyopewa,” alisema na kusisitiza kuwa wameanza kubomoa nyumba zao kupisha ujenzi wa kituo hicho.
Alisema nchi nyingi zilizoendelea zimefanikiwa kwa kutenga maeneo kama hayo ambayo yana viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.
Alisisitiza wawekezaji kutumia fursa hiyo maana eneo hilo linaandaliwa kwa ajili ya kituo cha kibiashara ambacho ndani yake kutajengwa viwanda ili bidhaa zipatikane hapa nchini kwa ghramna nafuu.
Kwa muda mrefu sasa serikali imekuwa katika juhudi za kupunguza gharama za kufanya biashara hapa nchini na wataalamu wanasema ujio wa kituo hiki ni moja ya hatua hizo.

Mwisho