Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) Bw. Aloyce Masanja
akiwaonyesha wadau kutoka katika taasisi na Idara mbalimbali za serikali ripoti
ya awali iliyotayarishwa na Kampuni ya
Odebretch International ya Brazili ikiwa ni hatua ya awali ya
utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maji wa Stierglers Gorge,
ripoti hiyo imewasilishwa kwa wadau hao ili kuijadili na kuangalia kama moja ya hatua za utekelezaji
mradi huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) Bw. Aloyce Masanja akiwaonyesha wadau kutoka katika taasisi na Idara mbalimbali za serikali ripoti ya awali iliyotayarishwa na Kampuni ya Odebretch International ya Brazili ikiwa ni hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maji wa Stierglers Gorge, ripoti hiyo imewasilishwa kwa wadau hao ili kuijadili na kuangalia kama moja ya hatua za utekelezaji mradi huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka hiyo, Profesa Raphael Mwalyosi.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto
Rufiji (RUBADA) imekutana na wadau mbalimbali toka idara na taasisi za serikali
kujadili ripoti ya awali ya ujenzi wa mradi wa Stieglers Gorge.
Hatua hiyo muhimu imefikiwa kama moja
ya michakato kuelekea utekelezaji wa mradi huo ambao utatekelezwa kwa
ushirikiano kati ya RUBADA na Kampuni ya Odebretch International ya Brazil.
“Tumejadili kwa mafanikio makubwa
ripoti hii ya awali na mwelekeo ni mzuri,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Bw.
Aloyce Masanja mbele ya waandishi wa
habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam mara baada ya mkutano huo.
Ripoti husika ilitayarishwa na
kampuni hiyo ya Brazil na kukabidhiwa kwa ungozi wa RUBADA miezi michache
iliyopita.
Ripoti hiyo inatoa picha kamili ya
mwelekeo wa utekelezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajiwa kuzalisha 2100MW za
umeme mara utakapokamilika.
Ripoti na mapendekezo hayo imegusa
maswala kama maji, teknolojia itakayotumika, vyanzo vya fedha na utunzaji wa
vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Bonde la Mto Rufiji linapita katika
mikoa nane na linakaliwa na watu milioni nane hivyo kukamilika kwa mradi huo
kutakuwa na msaada mkubwa katika shughuli za maendeleo.
Bw. Masanja aliwaambia waandishi wa
habari kuwa hatua ya kujadili ripoti hiyo ilikua ya muhimu sana kuelekea
utekelezaji wake maana utahusisha wadau mbalimbali.
“Kimsingi wajumbe hao wa mkutano
walikubaliana kuhusiana na umuhimu wa kutekelezwa kwa mradi huo,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Masanja, awamu ya
pili ya mradi huo itaanza April, 2013
kwa kuanza kufanya tathmini ya upembuzi yakinifu ya kimazingira ili kuchukua
tahadhari kulinda mazingira, viumbe na shuhghuli za kilimo cha umwagiliaji.
Pia awamu hiyo itaangalia namna ya ujenzi
wa mbiundombinu mbalimbali itakavyokuwa ikiwemo ya nguzo za umeme, na barabara
kutoka katika eneo la mradi hadi Chalinze mkoa wa Pwani.
Alisema awamu hiyo itakamilika Juni
2014 baada ya kukamilisha upembuzi huo yakinifu na kupata vibali mbalimbali vya
kuanzisha mradi huo vikiwemo vya matumizi ya maji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu,
sayansi na utamaduni (UNESCO) kwa sababu mradi upo katika hifadhi ya Selous.
Alisema ujenzi unatarajia kugharimu
dola za Kimarekani bilioni 2.3 ambapo ghrama halisi za mradi mzima ni dola za
kimarekani bilioni 3.6.
“Umeme huu ni muhimu katika
uzalishaji viwandani na migodini sababu
ni rahisi ambapo uniti moja itauzwa dola ya kimarekani senti nne ,” na kuongeza
kusema tayari masoko yako wazi na ni mengi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi RUBADA, Profesa Raphael Mwalyosi alisema mradi huo ni wa mseto na
unatarajia kuzalisha nishati ya umeme na pia utachochea kilimo cha umwagiliaji
Rufiji chini, maji ya kunywa na utalii katika hifadhi ya Selous.
“Mafanikio ya mradi huo unahitaji
ushirikiano mkubwa wa kutunza vyanzo vya maji kutoka TANESCO, DAWASA, Wizara ya
maji, Wizara ya Kilimo na Chakula na RUBADA,”alisema Profesa Mwalyosi.
Alisema umeme wa maji ni muhimu na ni
uwekezaji endelevu ukilinganisha na umeme wa vyanzo vingine pamoja na kwamba
kuna changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi,hivyo kuna kila sababu ya mradi huo
kukamilishwa.
Alisema viongozi na wadau mbalimbali
wanahitajika kuunga mkono ujenzi wa mardi sababu utasaidia kukua kwa uchumi wa
nchi na ustawi wa jamii.
Wadau walioshiriki kujadili ripoti hiyo
walitoka Wizara ya Nishati na Madini, Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji,
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, EWURA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, RUBADA
na taasisi mbalimbali.
Mwisho