Na Mwandishi wetu, Dar es
Salaam
Watanzania wamepewa
changamoto kuchangamkia miradi itakayotayarishwa chini ya utaratibu wa ubia
kati ya serikali na sekta binafsi (PPP) mara utekelezaji wake utakapokuwa tayari.
Wito huu umetolewa Meneja
wa kitengo cha uratibu wa mpango huo wa PPP, Bw. Saidi Amiri alipokuwa akiongea
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
“Sheria iliyounda mpango
huu inasisitiza sana uwezeshaji wa wananchi kwa njia ya kushirikishwa katika
miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema, akiongeza kwamba kwa sasa kitengo
hicho kiko katika hatua za kupitia miradi hiyo itakayogusa sekta mbalimbali.
Utaratibu huu utatekelezwa
kwa sheria namba 18 ya mwaka 2010.
Alisema miradi hiyo ya ubia
ikifanikiwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuunga mkono malengo ya taifa ya maendeleo
ya miaka mitano na dira ya taifa ya mwaka 2025.
Alisema kwa sasa wanafanya
upembuzi yakinifu wa miradi hiyo itakayohusisha sekta mbalimbali katika maeneo
ya miundombinu, kilimo na nyinginezo na kwamba kipaumbele kitakuwa kwa
wafanyabiashara wazawa watakaokuwa na uwezo.
Kitengo cha PPP kimeunda
na vitengo viwili; kile cha uratibu kilicho katika kituo cha Uwekezaji Tanzania
na kile cha fedha kilicho katika wizara ya Fedha.
Alisema Serikali kupitia wizara na taasisi
zake itaibua miradi ya ubia na kuifikisha kitengo cha uratibu TIC ambapo itachambuliwa kitaalamu na kuifikisha Wizara
ya fedha kwa ajili ya uhakiki wa mwisho.
Alisema baada ya hapo miradi
itatangazwa kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kupata wawekezaji kwa kushirikiana
na serikali.
Akielezea zaidi Bw. Amiri
alisema katika miradi ya namna hiyo mwekezaji anaweza kujenga barabara,bandari,
na viwanja vya ndege vizuri na vyenye viwango vya kimataifa na kuwatoza fedha
wanaotumia vitega uchumi hivyo.
Akitoa mfano alisema
mpango kama huu umesaidia sana kufikiwa kwa maendeleo makubwa katika nchi ya
Afrika Kusini hasa katika sekta ya miundombinu ya barabara.
Alisema kitengo hicho kilichoanzishwa
mwezi Machi mwaka huu kinazidi kutoa elimu kwa watumishi wa ummma na jamii kwa
ujumla ili kuwa na ufahamu zaidi juu ya swala hilo ili kufikia malengo yake.
Alisema kwa kuanzia katika
kila Wizara patakuwa na maafisa wa PPP na ili kusaidia kubuni miradi na
kuifikisha TIC iweze kufanyiwa upembuzi wa kitaalamu na kufikishwa Wizara ya
fedha.
Bw. Amiri alihamasisha
wawekezaji hasa taasisi za ndani za fedha kutumia fursa hiyo kuwekeza katika
miradi mbalimbali itakapokuwa tayari.
Mwisho
No comments:
Post a Comment