Monday, October 29, 2012

Miss Tanzania yazindua tovuti, yasisitiza umuhimu wa urembo


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Jamii imesisitizwa kuona shughuli za urembo kama fani nyingine ambayo ikifanywa vizuri inaweza kumkomboa mshiriki kiuchumi na kumuibua kama mtu wa muhimu katika jamii.

Wito huu umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Bw. Prashant Patel aliyekua mgeni rasmi katika uzinduzi wa tovuti ya mashindano hayo, www.misstanzaniatreasures.com, mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Lengo la tovuti hii ni kutaka kueneza elimu hiyo na kuonyesha kwamba urembo ni kazi au fani kama nyingine na wala haina uhusiano wowote na uhuni kama baadhi ya watu wanavyoendelea kuamini,” alisema Bw. Prashant.
Alisema wengi wa warembo waliowahi kufanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania leo hii ni watu wenye mafanikio makubwa, kila mtu akifanya kile anachokipenda na kukiweza. 
Alisema tovuti hiyo inataka kuwaibua siyo tu washindi wa Miss Tanzania waliopita, bali washiriki mbalimbali waliwahi kushiriki katika mashindano hayo na kuonyesha wako wapi, wanafanya nini, ndoto na matarajio waliyonayo na hata changamoto wanazokumbana nazo.
Hadi sasa kuna jumla ya washiriki zaidi ya elfu tano tangu Miss Tanzania ianzishwe mwaka 1994. 
Alisema kamati ya MissTanzania inaamini warembo hawa ni hazina na hivyo wanataka kuonyesha hazina iliyopo katika taifa.
Alisema juhudi hizi za kuanzishwa kwa tovuti hii zitafuatiwa na uanzishwaji wa jarida litakalojulikana pia kama Miss Tanzania Treasures.
Akielezea zaidi alisema sehemu ya faida itakayotokana na tovuti hii na jarida hilo itatumika katika kuchangia maendeleo ya warembo hawa kama elimu na shughuli mbalimbali wanazofanya kwa utaratibu utakaopangwa.  Pia, faida itakayopatikana itatumika katika kusaidia watoto yatima hapa nchini.
“Tovuti hii itasaidia dunia nzima kushuhudia na kujua kwa undani kuhusu Miss Tanzania.  Hii ni fursa nyingine katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini maana hakuna ubishi kwamba Miss Tanzania imekua moja ya njia za kukuza utalii wetu nje ya nchi,” alisisitiza.
Akielezea zaidi alisema tovuti ni njia muafaka katika kipindi hiki cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo maendeleo yanategemea zaidi ufanisi katika mawasiliano.
“Tovuti hii itasaidia kujenga mtandao baina ya warembo wenyewe na wakajua jinsi ya kushirikiana katika maswala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuchochea maendeleo,” alisema.
Alisisitiza kuwa tovuti hii pia itasaidia kujenga mahusiano na mawasiliano kati ya warembo wa Miss Tanzania kwa upande mmoja  na wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi.
“Tutawashirikisha wadau mbalimbali katika swala hili muhimu na ni wito wetu kwamba wasituangushe kwa faida ya nchi yetu,” alisema Bw. Prashant.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa tovuti hiyo, Bw. Ali Zoeb aliwaahidi warembo walioshiriki uzinduzi huo kuwa tovuti hiyo itasaidia sana katika kuwaunganisha na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuwasisitiza warembo popote walipo kuanza kujenga mazoea ya kutembelea tovuti hiyo na kujua kinachojiri.

Naye, mshauri wa habari wa tovuti hiyo, Bw. Peter Keasi alisema tovuti na jarida litakaloanzishwa hivi karibuni vitasaidia kurahisisha mawasiliano kufanya kazi kama daraja baina ya warembo hapa nchini, jambo alilosema ni muhimu kwa maendeleo.

Uzinduzi huo ulishuhudiwa na warembo walioko kwenye kambi ya Miss Tanzania kwa sasa pamoja na wadau wengine wa urembo hapa nchini.

Mwisho 

No comments: