Wednesday, May 6, 2015

Ulinzi wa kutuma mbwa bandarini, uwanja wa ndege mbioni kuanza

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani imezindua programu ya uimarishaji ulinzi katika bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa Ndege wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kutumia mbwa maalumu kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu.

Wizara zinazohusika na programu hiyo hapa nchini ni pamoja na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema programu hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo kwa kuanzia ili kupambana na wasafirishaji wa madawa ya kulevya na pembe za ndovu.

“Tumedhamiria kupambana na wahalifu hawa hadi mwisho,” alisema.
Chini ya mpango huo, polisi wa Tanzania watapatiwa mafunzo nchini marekani ya kutumia mbwa maalumu kwa ajili ya kuanza kutumia mbwa hao maalum katika maeneo hayo ifikkapo mwezi Septemba mwaka huu.


Waziri alisema dhamira ya serikali ni kuwa na ulinzi wa namna hiyo katika mipaka yote ya nchi kuhakikisha taifa linakuwa salama kutokana na uharibifu unaofanywa na watu wasio na mapenzi mema na taifa lao.

Thursday, March 26, 2015

Maeneo huru ya uwekezaji yapewe msaada unaotakiwa -TNBC

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Mhandisi Raymond Mbilinyi (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Global Industrial Park Ltd, Bw. Zainuddin  Adamjee muda mfupi mara baada ya kumaliza kwa kikao cha baraza la biashara la mkoa wa pwani hivi karibu mjini Bagamoyo.  Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau toka sekta ya umma na binafsi.
Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
Baraza la Biashara la mkoa wa Pwani limetakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji waliowekeza katika maeneo maalumu ya ukanda wa uwekezaji mkoani humo.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Mhandisi Raymond Mbilinyi amesema hivi karibuni mkoani hapa kuwa maeneo maalum ya ukanda ya uwekezaji ni njia bora ya kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama yataendelea kwa kiwango kinachotakiwa.

“Nchi nyingi zimefikia maendeleo kwa kutumia njia hii ya kuwekeza katika maeneo maalum, kama baraza la mkoa ni muhimu mkahakikisha yanaendelea bila tatizo,” alisema.

Akiongea katika kikao cha baraza la mkoa huo hivi karibuni mjini Bagamoyo, alisema ukanda huo maalumu katika mji huo utasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa ajira pamoja na kuinua kipato cha wakazi wa mji huo.


“Sasa hivi kuna tatizo la ajira katika miji yetu, hivyo uwepo wa viwanda utasaidia vijana wengi kupata ajira,” aliongeza.

Huduma TPA kuimarika kufuatia kujiunga na mkongo wa mawasiliano

Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Killiani Chale (kushoto) akipokea cheti cha Mamlaka hiyo kuunganishwa na mkongo wa mawasiliano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ambapo matawi 13 ya mamlaka hiyo yameunganishwa na mfumo huo wa mawasiliano.  Hafla hiyo iliambatana na mamlaka hiyo kukabidhiwa mradi huo baada ya kukamilika.  Kulia ni Ofisa Mkuu wa Ufundi wa TTCL, Bw. Senzige Kisenge.  Tukio hilo lilifanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Huduma za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) zinatarajiwa kuimarika kufuatia hatua ya makao makuu ya mamlaka hiyo kuunganishwa kupitia teknolojia ya kisasa na matawi yake 13 nchini.

Mradi huo uliokwishaanza kutekelezwa unafuatia kuunganishwa kwa TPA na mkongo wa mawasiliano wa Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) kupitia mfumo unaoitwa Multiprotocal Label Switching Virtual Private Network (MPLS VPN).
Kupitia mfumo huo wa MPLS VPN, huduma za sauti, data na intaneti za TPA zinatarajiwa kuimarika kwa kiwango kikubwa.

“Mradi huu uliotekelezwa na TTCL utatusaidia kuimarisha huduma za bandari zetu pamoja na wateja wetu,” Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa TPA, Bw. Killian Chale alisema wakati wa kukabidhiwa rasmi mradi huo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Matawi ya TPA yaliyounganishwa na mfumo huo wa mawasiliano ni pamoja na ofisi ya makao makuu TPA, bandari za Mwanza, Kigoma, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam, Mafia, Lindi, Kilwa, Pemba, Bukoba, Nansio na Musoma.


Kwa mujibu wa Bw. Chale, sasa mawasiliano kati ya bandari moja na nyingine yatatumia mfumo wa CISCO ambao ni wa gharama nafuu na usikivu wake ni bora zaidi.