Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa wito
kwa wafanyabiashara watanzania kuanza kutumia alama ya kiambishi
anuani (Barcodes) ya hapa nchini kwa faida yao na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu alitoa wito huo jana
jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mpango mkakati wa miaka mitano 2013/2017
wa GSI (TZ) National Ltd.
GSI (TZ) National Ltd ndio
inayohusika na mfumo wa kimataifa wa utambuzi na bidhaa kwa kutumia nembo za
mstari (Barcodes).
“Nchi yetu imeingia katika mfumo huu
ambao utasaidia kuimarisha ushindani wetu katika soko la ndani na nje,”
alisema.
Tanzania ilifanikiwa kuingia katika
mfumo huo baada ya kutimiza mashari ya kuwa mawanachama wa Global Standard One
(GS1) yenye makao makuu yake nchini Ubelgiji.
Alama ya kiambishi anuani au barcode
husaidia kutambulisha bidhaa husika katika soko na kwa muda mrefu Tanzania
imekuwa ikitumia alama za nchi nyingine katika bidhaa zake.
Hata hivyo, kuanzia mwezi Agosti
2011, Tanzania kupitia GS1 (TZ) National Ltd ilifanikiwa kuanza kutoka alama
hiyo, hatua inayotegemewa kuongeza kuaminika kwa bidhaa za hapa nchini kitaifa
na kimataifa na hivyo kuchochea kukua kwa uchumi wa wafanyabiashara pamoja na
nchi.
Namba ya utambulisho ya alama ya
kiambishi anuani ya Tanzania ni 620.
Waziri Mkuu Pinda alisema ni muhimu
kwa wafanyabiashara wote sasa kuingia katika mfumo huo kwani utawawezesha
kuingia kwa ufanisi zaidi na kushindana katika masoko ya kimataifa.
“Natoa wito kwa wafanyabiashara ambao
bado hawajaingia na wale wanaoendelea kutumia nembo za barcodes za mataifa
mengine kuacha kufanya hivyo kwa vile taifa lina nembo yake,”alisema.
Aliitaka GSI (TZ) National Ltd kutumia
mpango mkakati wake wa miaka mitano kujitangaza kwa nguvu zote ili
wajasiriamali na wafanyabiashara wote waweze kuingia katika mfumo huo wa
kimataifa kwa vile una faida kubwa kwao.
“Ni jambo la kujivunia kuwa wazalishaji
370 wameingia katika mfumo wa kuwa na barcodes na jumla ya bidhaa 6,000
zilizopo sokoni nazo zina alama hii hadi sasa,”alisema Bw. Pinda.
Alifafanua kwamba serikali ya awamu
ya nne ilifanya juhudi kubwa kupata alama hiyo ya utambulisho ili kama moja ya
juhudi za kuimarisha sekta binafsi na wajasiriamali hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Esther Mkwizu alisema Tanzania
imefanikiwa kufika hapo kutokana na juhudi za pamoja kati ya serikali na sekta
binafsi na sasa bidhaa za Tanzania zina utambulisho.
“Ili kuleta mafanikio zaidi ya mfumo
huu, serikali inahitajika kuweka sera bora ya kuuendeleza na isaidie
wafabiashara wote kujiunga na mfumo huo ili kuchochea uzalishaji katika sekta
za viwanda na kilimo,” alisema.
Alisisitiza kuwa wale walio na alama
hiyo tayari wanahitajika kuwa mabalozi wazuri katika matumizi yake ili
kuhamasisha wale ambao hawajaingia katika mfumo huo
Makamu Mwenyekiti wa GSI (TZ)
National Ltd, Bw. Yakub Hasham alisema Tanzania imefanya mapinduzi makubwa ya
kuwa na alama yake ambayo itasaidia kuzitambulisha bidhaa zahapa nchini katika
masoko mbalimbali.
Mwisho