Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Jamii imesisitizwa kuona shughuli za urembo kama fani nyingine ambayo
ikifanywa vizuri inaweza kumkomboa mshiriki kiuchumi na kumuibua kama mtu wa
muhimu katika jamii.
Wito huu umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Bw. Prashant
Patel aliyekua mgeni rasmi katika uzinduzi wa tovuti ya mashindano hayo, www.misstanzaniatreasures.com,
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Lengo la tovuti hii
ni kutaka kueneza elimu hiyo na kuonyesha kwamba urembo ni kazi au fani kama
nyingine na wala haina uhusiano wowote na uhuni kama baadhi ya watu
wanavyoendelea kuamini,” alisema Bw. Prashant.
Alisema wengi wa warembo
waliowahi kufanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania leo hii ni watu wenye
mafanikio makubwa, kila mtu akifanya kile anachokipenda na kukiweza.
Alisema tovuti hiyo
inataka kuwaibua siyo tu washindi wa Miss Tanzania waliopita, bali washiriki
mbalimbali waliwahi kushiriki katika mashindano hayo na kuonyesha wako wapi,
wanafanya nini, ndoto na matarajio waliyonayo na hata changamoto wanazokumbana
nazo.
Hadi sasa kuna jumla
ya washiriki zaidi ya elfu tano tangu Miss Tanzania ianzishwe mwaka 1994.
Alisema kamati ya
MissTanzania inaamini warembo hawa ni hazina na hivyo wanataka kuonyesha hazina
iliyopo katika taifa.
Alisema juhudi hizi za
kuanzishwa kwa tovuti hii zitafuatiwa na uanzishwaji wa jarida litakalojulikana
pia kama Miss Tanzania Treasures.
Akielezea zaidi
alisema sehemu ya faida itakayotokana na tovuti hii na jarida hilo itatumika
katika kuchangia maendeleo ya warembo hawa kama elimu na shughuli mbalimbali
wanazofanya kwa utaratibu utakaopangwa.
Pia, faida itakayopatikana itatumika katika kusaidia watoto yatima hapa
nchini.
“Tovuti hii itasaidia
dunia nzima kushuhudia na kujua kwa undani kuhusu Miss Tanzania. Hii ni fursa nyingine katika kukuza sekta ya
utalii hapa nchini maana hakuna ubishi kwamba Miss Tanzania imekua moja ya njia
za kukuza utalii wetu nje ya nchi,” alisisitiza.
Akielezea zaidi
alisema tovuti ni njia muafaka katika kipindi hiki cha Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ambapo maendeleo yanategemea zaidi ufanisi katika
mawasiliano.
“Tovuti hii itasaidia
kujenga mtandao baina ya warembo wenyewe na wakajua jinsi ya kushirikiana
katika maswala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuchochea maendeleo,”
alisema.
Alisisitiza kuwa tovuti
hii pia itasaidia kujenga mahusiano na mawasiliano kati ya warembo wa Miss
Tanzania kwa upande mmoja na wadau wa
maendeleo ndani na nje ya nchi.
“Tutawashirikisha
wadau mbalimbali katika swala hili muhimu na ni wito wetu kwamba wasituangushe
kwa faida ya nchi yetu,” alisema Bw. Prashant.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa tovuti hiyo, Bw. Ali Zoeb aliwaahidi
warembo walioshiriki uzinduzi huo kuwa tovuti hiyo itasaidia sana katika
kuwaunganisha na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuwasisitiza warembo
popote walipo kuanza kujenga mazoea ya kutembelea tovuti hiyo na kujua
kinachojiri.
Naye, mshauri wa habari wa tovuti hiyo, Bw. Peter Keasi alisema tovuti na
jarida litakaloanzishwa hivi karibuni vitasaidia kurahisisha mawasiliano
kufanya kazi kama daraja baina ya warembo hapa nchini, jambo alilosema ni
muhimu kwa maendeleo.
Uzinduzi huo ulishuhudiwa na warembo walioko kwenye kambi ya Miss Tanzania
kwa sasa pamoja na wadau wengine wa urembo hapa nchini.
Mwisho