Wednesday, May 6, 2015

Ulinzi wa kutuma mbwa bandarini, uwanja wa ndege mbioni kuanza

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani imezindua programu ya uimarishaji ulinzi katika bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa Ndege wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kutumia mbwa maalumu kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu.

Wizara zinazohusika na programu hiyo hapa nchini ni pamoja na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema programu hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo kwa kuanzia ili kupambana na wasafirishaji wa madawa ya kulevya na pembe za ndovu.

“Tumedhamiria kupambana na wahalifu hawa hadi mwisho,” alisema.
Chini ya mpango huo, polisi wa Tanzania watapatiwa mafunzo nchini marekani ya kutumia mbwa maalumu kwa ajili ya kuanza kutumia mbwa hao maalum katika maeneo hayo ifikkapo mwezi Septemba mwaka huu.


Waziri alisema dhamira ya serikali ni kuwa na ulinzi wa namna hiyo katika mipaka yote ya nchi kuhakikisha taifa linakuwa salama kutokana na uharibifu unaofanywa na watu wasio na mapenzi mema na taifa lao.