Tuesday, December 16, 2014

ZANTEL yasaidia michezo ya ngumi, karate

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya simu za mkononi ZANTEL, Bw. Pratap Ghose akisalimiana na bondia maarufu, Francis Cheka wakati kampuni hiyo ilipokabidhi ulingo wa kisasa wa mchezo wa ngumi kwa serikali hivi karibuni.  Kulia ni Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni, Fenela Mukangara.
Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni, Fenela Mukangara akiwa amevaa vifaa vya mchezo wa ngumi wakati wa makabidhiano ya ulingo wa kisasa wa mchezo wa ngumi kwa serikali hivi karibuni.  Kushoto ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya simu za mkononi ZANTEL, Bw. Pratap Ghose.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Kampuni ya simu za mkononi, ZANTEL imetoa msaada kwa serikali wa ulingo mpya wa kisasa wa mchezo wa ngumi kama moja ya njia za kuendeleza sekta ya michezo nchini.

Akiongea wakati wa makabidhiano hayo jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Pratap Ghose alisema wao wanaamini kuwa michezo ina mchango mkubwa na muhimu kwa taifa.

“Ukipewa umakini na uwekezaji unaotakiwa, mchezo wa ngumi unaweza kuwa chanzo cha ajira kwa vijana na kutangaza nchi nje,” alisema.

Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni, Dk. Fenela Mukangara alipokea msaada huo kwa niaba ya serikali.


Bw. Pratap aliahidi kuwa kampuni yake itaendelea kusaidia serikali kuhakikisha kuwa wachezaji wa Tanzania wanawezeshwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

TCCIA yaongeza faida mara dufu

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya uwekezaji (TCCIA), Mhandisi Aloys Mwamanga (katikati) akisisitiza jambo wakati  wa mkutano mkuu wa tisa wa mwaka wa kampuni hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. kulia ni Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Donald Kamori na Makamu Mwenyekiti, Bw Joseph Kahungwa.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya uwekezaji (TCCIA), Bw. Donald Kamori (kulia) akiteta jambo na mmoja wa wanahisa wa kampuni hiyo, Bw. Arphaxad Masambu wakati  wa mkutano mkuu wa tisa wa mwaka wa kampuni hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. 
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya Uwekezaji TCCIA imeelezea kupata faida zaidi katika mwaka 2014 kulinganisha na mwaka uliopita.

Kwa mwaka huu, kampuni hiyo imepata mafanikio makubwa ya uendeshaji ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu inatarajia kupata faida ya Tshs milioni 523, 651, 788 ukilinganisha na Tshs milioni 411,763, 328 iliyopata mwaka 2013.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Donald Kamori alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa tisa wa mwaka mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

“Mafanikio haya yanatokana na utendaji mzuri na ushirikiano kati ya bodi na menejimenti yetu... tutaendelea kufanya hivyo kwa mwaka unaokuja,”alisema.


Alisema mafanikio hayo pia yamechangiwa na uwekezaji mzuri ambao umefanywa kwenye kampuni zinazojiendesha kwa faida na zinazolipa gawio la hisa kila mwaka.