Tuesday, November 25, 2014

Sheria, sera ya kazi tatizo kwa waajiri

Arusha
Imeelezwa kuwa waajiri kutofahamu vyema Sera ya Kazi ya mwaka 2008 na sheria ya Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO), husababisha migogoro kazini.

Mkurugenzi wa elimu wa shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Edwin Mwakyembe alisema hayo katika mafunzo ya wajasiriamali na waajiri yaliyofanyika Arumeru.

Mwakyembe alisema waajiri, wafanyakazi na wajasiriamali wadogo wana wajibu wa kuzifahamu sheria za kazi.

Alisema shughuli za wajasiriamali pia ni muhimu kwa kuwa zinasaidia kupunguza umaskini kwenye jamii.

Ofisa kazi mkuu kutoka Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Baltazar Mushi alisema Serikali inatekeelza mikataba ya kazi ya kimataifa iliyoiridhia, kama toleo la Sheria ya Kazi lililotolewa kwa lugha rahisi ili kuwezesha waajiri na waajiriwa kutumia.

“Sheria inapotungwa ina maana tatu. Inakusudia jambo Fulani lifanyike au lisifanyike, hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza migogoro ambayo mara nyingi inaibuka na kuzorotesha uzalishaji mali.


Mwanga wamshukuru Prof. Maghembe, serikali kwa mabati

Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe (katikati) akitoa maelekezo kwa baadhi ya watendaji wa vijiji vilivyoathirika na mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka 2013 Wilayani Mwanga mkoani Kilimanjro wakati wa zoezi la kugawa mabati kwa wathirika hao.  kushoto ni mratibu wa maafa wilaya ya Mwanga, Kiluvia Mzighani na kulia ni mmoja wa wazee walioathirika na mafuriko hayo Elia Msuya.
 
Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto) akimkabidhi mabati Bi. Evalista Yese (wa pili kulia) kutoka katika kijiji cha Mwaniko kata ya mwaniko wilayani mwanga mkoani Kilimanjaro hivi karibuni ambae ni mmoja wa waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka 2013 wilayani humo.  Kushoto ni mkuu wa wilaya ya Mwanga, Shwaiba Ndemanga.
Na Mwandishi Wetu, Mwanga

Wananchi waishio katika vijiji vya Vungi, Ubani, Vuchama Ngofi, Mriti na Mwaniko katika kata za Mwaniko na Kifula wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameishukuru serikali kwa msaada wa mabati.

Msaada huo wa mabati ulitolewa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwanzoni mwa mwaka 2013 na kusababisha kaya zaidi ya 796 kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.

Mabati hayo zaidi ya 2300 yametolewa na mbunge huyo, serikali pamoja na wadau wengine waliochangia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni mara baada ya kukabidhiwa mabati na mbunge wa Mwanga ambaye pia ni waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe,  wananchi hao walisema kuwa wamepata faraja kubwa baada ya kuona kilio chao kimesikika.

“Tunashukuru kwa hili, tulikua tunalala kwa majirani na mara nyingine hata nje,” alisema Gadi Msuya kutoka kijiji cha Vuchama Ngofi.

Naye Evalista Yese kutoka katika kikiji cha Mwaniko, alisema serikali imefanya jambo kubwa sana, huku akimshukuru mbunge wa jimbo hilo kwa juhudi kubwa aliyoifanya katika kutekeleza ahadi aliyowapa ya kuwapelekea mabati.

“Kati ya vitu vikubwa alivyofanya mbunge wetu katika kipindi hiki kigumu ni hili la kuleta mabati kwa wana Mwaniko,” alisema Evalista.


Monday, November 24, 2014

Wasomi wamuenzi Mwalimu kwa vitendo—Prof. Kamuzora

Na Mwandishi wetu, Morogoro
Changamoto imetolewa kwa wasomi nchini kutumia taaluma zao kubuni njia zitakazoleta suluhisho la matatizo na changamoto mbalimbali za wananchi na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa naibu makamu mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawala na Fedha, Profesa Faustin Kamuzora, ni kwa kuchukua hatua madhubuti za kutumia taaluma zao kusaidia jamii ndipo wasomi hao watakuwa wamemuenzi hayati baba wa Taifa kama inavyotakiwa.

Alikuwa akiongea hivi karibuni wakati wa Kongamano la siku ya kumuenzi hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere liloandaliwa na chuo hicho mjini Morogoro.

“Taaluma zetu zitumike kutafuta majawabu ya sera na uvumbuzi wa aina mbalimbali ambao utasaidia kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni,”alisema.

Alisema watu wengi wamekuwa wakijipambanua kwa usomi wao lakini hawakumbuki kuwa wana deni kwa jamii la kuwaletea majawabu ya matatizo yao kupitia taaluma hizo.

“Kazi zetu zituonyeshe kuwa sisi ni wasomi,”alisema.

Alisema hakuna faida ya kujiita msomi wakati hakuna jambo hata moja la kitaaluma ambalo mtu amelifanya kwa ajili ya taifa.

Alisema wakati nchi inapomkumbuka baba wa taifa, ni vyema wasomi wakaiga mfano wake, kwani aliweza kuonyesha mfano kwa vitendo, kuongoza nchi kwa uadilifu uliotukuka na kuandika vitabu mbalimbali.


“Tuige mfano wa baba wa taifa kwa kutenda na kazi zetu zionekane na kuleta faida kwa jamii zetu na taifa kwa ujumla,” alisema.