Monday, August 18, 2014

Kongamano la biashara Marekani laanza kuzaa matunda -EPZA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Aldelhem Meru, akisisitiza jambo kwa waandishi mwishoni mwa wiki kuhusu kongamano la biashara lilofanyika nchini Marekani hivi karibu na kusema kuwa matunda yameanza kuoneka.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kongamano la maswala ya biashara lililofanyika nchini Marekani  mapema mwezi huu limeanza kuzaa matunda.

Sasa, wawekezaji kutoka nchi hiyo wameanza kutaka kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali kwenye maeneo maalumu yaMamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA).

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dr. Adelhelm Meru aliwaambia wandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa kongamano hilo lililojulikana kama “Doing Business in Tanzania” limeanza kuzaa matunda ya kupata wawekezaji kuwekeza katika maeneo yake maalumu.

“Katika siku chache baada ya kurejea, tumepata kampuni tatu ambazo zimeleta maombi ya nia ya moja kwa moja kuwekeza katika maeneo maalumu,”alisema.

Alisema mamlaka imepokea maombi yanayotaka kuwekeza katika maeneo ya kuongezwa thamani zao la ngozi, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), na ujenzi wa miundombinu katika maeeneo maalumu ya mamlaka.

Akifafanua zaidi alisema matarajio yaliyopo kwa sasa ni kuendelea kupata wawekezaji wengi toka nchi hiyo kwa vile kongamano hilo liliipa nafasi nzuri Tanzania kutangaza fursa zilizopo nchini.

Rais Jakaya Kikwete aliongoza ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo kubwa.

“Walionesha nia ya kutaka kuwekeza katika maeneo ya viwanda vya kuongeza thamani mazao ya Kilimo na uzalishaji nishati,” alifafanua Dk. Meru.

Alitaja maeneo mengine kama utafiti wa gesi na mafuta, utoaji wa huduma kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika bahari ya Hindi.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na watu zaidi ya 400 ambapo kampuni kubwa kutoka majimbo mbalimbali ya nchi humo zilishiriki ambapo wafanyabiashara wa Tanzania waliweza kukutana na wenzao wa Marekani na kuzungumza biashara.

“Wengi walitumia fursa hiyo kupata wabia, kuzungumza na kampuni zinazotoa mikopo na kupata masoko ya bidhaa za Tanzania,”alisema.

Kongamano hilo lilifanyika baada ya Rais Kikwete kushiriki mkutano wa Marais wa Afrika na Rais Barack Obama wa Marekani jijini Washngton D.C.

Kongamano hilo liliandaliwa na EPZA, Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na kituo cha uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kushirikiana na Corporate Council on Africa ya Marekani.


Mwisho

Vitambulisho vya taifa haviwezi kutumika kupiga kura--NEC

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kwa hali ilivyo sasa Watanzania hawawezi kutumia vitambulisho vya uraia kupiga kura, isipokuwa  tu  kadi  zitakazotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC).

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba, amefafanua jana jijini Dar es Salaam kwamba ni makosa kudhani   kuwa vitambulisho vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) vinaweza kutumika kupiga kura.

“Haiwezekani kabisa,” amesisitiza Bw. Mallaba na kuongeza ”tunaomba watu waelewe kuwa kadi za kupiga kura na vitambulisho vya uraia ni vitu viwili tofauti. Vitambulisho vya taifa siyo mbadala wa kadi za kupiga kura.”

Ameeleza kuwa kwa hali ilivyo utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa nchi nzima utachukua muda mrefu.  Watu wengi watakuwa hawajapata vitambulisha vya taifa hata baada ya chaguzi zilizoagizwa kisheria kupita.

Mkurugenzi ametoa ufafanuzi huo kufuatia taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba mtu asiye na kadi  ya kupiga kura anaweza kutumia kitambulisho cha uraia kupiga kura.

Alisema wakati uandikishaji wa NEC unafanyika kwa muda maalum ili kuwahi upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu, uandikishaji wa NIDA hauna muda maalum.

“NEC ina mchakato mfupi wa ukusanyaji wa taarifa za watu wanaoandikishwa na kadi za mpiga kura zinatolewa hapo hapo kituoni baada ya ujazaji wa fomu,” alisema.

Alisema kwa upande wa NIDA, mchakato wa ukusanyaji wa taarifa una utaratibu mrefu kutokana na wahusika zoezi hilo kuwa wengi.

Akielezea zaidi alisema namba ya kadi inayotolewa na NEC ni ya kipekee kwa mtu anayeandikishwa wakati NIDA inaweza kutoa namba zaidi ya moja endapo itabidi kutoa kitambulisho kingine kwa mtu huyo huyo kutokana na kitambulisho cha awali kupotea au kuharibika.

Bw. Mallaba alisema hata kama vitambulisho vya raia vingekuwa tayari, bado tume ingetakiwa kuandaa daftari kwa kuwa vitambulisho vya uraia huwa haviainisha mtu ni mpiga kura wa eneo gani.

“Ukipewa kitambulisho kile utajua huyu ni raia wa Tanzania lakini atakuwa hajaainishwa kwamba huyu ni mpiga kura wa jimbo  fulani  kwa maana ya ubunge au wa kata fulani kwa maana ya udiwani,” alisema.

Alifafanua kuwa  kama wananchi wote wangekuwa na vitambulisho vya taifa, kitu ambacho kingefanyika ni kwa tume kununua kifaa kinachoweza kusoma kitambulisho na kupata taarifa za muhusika na kumpangia muhusika sehemu yake ya kupigia kura.

Alisema swala la kufahamu eneo la wapiga kura na idadi ni la msingi sana katika kufanya maandalizi ya uchaguzi.

“Hata siku ya uchaguzi wenyewe, bila kuelewa kwamba sehemu fulani ina wapiga kura idadi fulani itakuwia vigumu sana kufanya kazi,” alisema.

Alifafanua kuwa hata vyama vya siasa navyo vitapenda hata kabla ya siku ya uchaguzi wafahamu eneo fulani lina wapiga kura wangapi.

“Ni kitu muhimu sana katika demokrasia ya uchaguzi kwa chama kuelewa  katika sehemu fulani kutakuwa na wapiga kura idadi fulani,” alisema, na kuongeza kuwa hata sheria inaitaka NEC siku kadhaa kabla ya uchaguzi kuonyesha idadi ya wapiga kura, majina katika maeneo yao.

Alisema hakuna nchi ya kiafrika inayotumia kitambulisho cha taifa moja kwa moja katika kupiga kura isipokuwa kutumika kurahisisha utaratibu wa kuandaa daftari la kudumu la wapiga kura.

“Kuwa na daftari hakuepukiki,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema uandikishaji wa vitambulisho vya taifa kwa upande mmoja na vitambulisho vya wapiga kura kwa upande mwingine ni shughuli mbili tofauti lakini zinazohusiana kwa karibu na pia zinazohusu wananchi.

“Watanzania wanaokuja mbele ya tume ni wachache kuliko wale wanaoenda kwenye mamlaka inayohusika na vitambulisho vya taifa,” alisema.
Alieleza kuwa zoezi la vitambulisho va uraia litakapokamilika litarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za raia zitakazosaidia matayarisho ya uchaguzi.

“Hakuna mgongano kati ya NIDA na NEC,” alisema.


Mwisho

Tuesday, August 12, 2014

NEC yafafanua kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
  
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kuanza hivi karibuni linamhusu kila raia mwenye sifa ya kupiga kura.

Ufafanuzi huu unakuja wakati pakiwa na mawazo tofauti ya nani hasa anatakiwa kushiriki katika zoezi hilo huku baadhi ya watu wakidhani kuwa jambo hili linawahusu wale ambao hawakupata kujiandikisha kupiga kura au waliopoteza kadi au waliofikia umri wa kupiga kura.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva amesema jana jijini Dar es Salaam kuwa katika kufanya maboresho hayo na kupata daftari linaloaminika zaidi, Tume inatarajia kutumia mfumo mpya wa “Biometric Voters Registration System” au mfumo ambao utatumia utambuzi wa watu kwa alama za binadamu.

Kwa kutumia mfumo huu, muhusika atachukuliwa alama za vidole vyote vya mikono 10, picha na sahihi yake.

Hii ni tofauti na mfumo uliokuwa unatumika wa “Optical Mark Recognition” (OMR) ambapo muhusika alikuwa anajaza fomu na kuchukuliwa alama ya kidole kimoja tu ambao Jaji Lubuva anasema ulikuwa na uwezekano wa watu kujiandikisha hata mara mbili bila kutambulika.

“Watu wote wenye sifa watatakiwa kujiandikisha upya katika mfumo huu mpya na kupatiwa kadi mpya,” alisema.

Akitoa ufafanuzi zaidi alisema uboreshaji wa daftari hilo unatokana na matakwa ya kisheria na malalamiko ya wadau mbalimbali.

Alisema tangu kufanyika kwa uchuguzi mkuu mwaka 2010 pamekuwa na malalamiko toka kwa wadau mbalimbali kama vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wapiga kura wenyewe kuhusu haja ya kuboresha daftari hilo na kuondoa watu ambao hawastahili kuwamo kama waliofariki na kuongeza wengine wenye sifa.

“Malalamiko haya yanafanya imani ya watu juu ya daftari la wapiga kura iwe ndogo,” alisema.

Alifafanua kuwa sheria inaitaka NEC kuboresha daftari la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi uliopita na uchaguzi unaokuja.

“Ni kutokana na matakwa ya kikatiba na sheria na malalamiko haya, NEC imelazimika kufanya zoezi hili kabla ya kura ya maoni na uchaguzi mkuu ujao 2015,” alisema.

Akizungumzia matayarisho ya zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba alisema yanaridhisha na kuendelea vizuri.

Alisema maboresho ya daftari hilo kwa awamu hii ni mahsusi kwa ajili ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya mapema mwaka 2015, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 pamoja na chaguzi ndogo zitakazofuata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Sehemu kubwa ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yamekamilika,” alisema.

Akielezea zaidi Bw. Mallaba alisema tayari NEC imeanzisha na kuhakiki vituo vipya na kuviweka katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa.

Vituo hivyo vimeongezeka kutoka vituo vya awali 24,919 na kufikia vituo 40,015 nchi nzima.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari ununuzi wa vifaa vya uandikishaji ikiwemo Biometric Voter Registration Kits umeshafanyika.

“Maandalizi ya melekezo kwa maafisa waandikishaji, waandishi wasaidizi pamoja na vyama vya siasa yameshafanyika,” alisema na kuongeza kuwa kanuni za uboreshaji zimeshaandaliwa.

Alisema kuwa maandalizi ya kituo cha kuhifadhia taarifa na mkakati wa utoaji wa elimu ya mpiga kura na machapisho mbalimbali tayari yameshakamilika.

Aliongeza kuwa katika maandalizi hayo, Tume imeshakutana na wadau mbalimbali kama wahariri, viongozi wa dini na vyama vya siasa ili kujadiliana na kupata maoni yao kuhusiana na zoezi hilo.

“Tunashukuru sana kwa michango ya mawazo yao…tunayapokea na kuyafanyia kazi,” alisema na kuongeza kuwa katika kuboresha zaidi, Tume inatarajia kukutana na makundi mengine kama vijana, kina mama na walemavu.

NEC imepewa jukumu la kisheria kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura na kuliboresha daftari hilo kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwisho