Tuesday, August 12, 2014

TNBC yawataka watendaji Iringa kujenga mazingira bora ya uwekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma akizungumza wakati wa mkutano wa siku moja wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa hivi karibuni.  Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe kutoka sekta ya umma na binafsi na kuzungumzia namna ya kuimarisha mazingira bora ya biashara na uwekezaji mkoani humo. 
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akizungumza na wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa kwenye mkutano wa siku moja uliowakutanisha wajumbe wa sekta ya umma na binafsi na kuzungumzia namna ya kuimarisha mazingira bora ya biashara na uwekezaji mkoani humo hivi karibuni.  Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Ramadhani Mungi (kushoto).
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. Christine Ishengoma akizungumza jambo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Bw. Raymond Mbilinyi baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku moja wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa hivi karibuni.  Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe kutoka sekta ya umma na binafsi na kuzungumzia namna ya kuimarisha mazingira bora ya biashara na uwekezaji mkoani humo. 
Na Mwandishi Wetu, Iringa

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limewataka watendaji wa halmashauri zilizopo katika mkoa wa Iringa kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuweza kuwavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw. Raymond Mbilinyi amesema mkoani humo wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la biashara la mkoa wa Iringa juu ya mikakati mbalimbali ya kuimarisha uchumi na kujenga mazingira bora ya biashara katika mkoa huo.

“Watendaji siku zote ndio wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kusaidia serikali katika suala la uwekezaji katika halmashauri zao,” alisema Mbilinyi.

Alisema kazi kubwa ya baraza ni kuunganisha sekta binafsi na ile ya umma kuhakikisha wanafanya kazi pamoja hivyo ni jukumu la watendaji wa ngazi za juu katika halmashauri hizo kujenga mazingira bora ya biashara ili kuvutia wawekezaji wengi.

“Bila kuboresha mazingira, hamna biashara wala uwekezaji,” alisema.

Alisisitiza kuwa Baraza litaendelea kukutana na wajumbe wa upande wa sekta ya umma na binafsi ili kujadiliana kama kuna vikwazo vyovyote katika ufanyaji biashara ili kuweza kuvitatua kama si kuviondoa kabisa.

“kumekuwa na vikwazo katika ufanyaji biashara hivyo mikutano kama hii ni muhimu sana katika kutatua kero mbalimbali,” alisisitiza Bw. Mbilinyi.

Akielezea umuhimu wa mabaraza hayo, alisema ni mkubwa kwa kuwa wajumbe wa pande zote mbili hukutana na kutoka na kauli moja ya kutatua kero ambazo zipo katika biashara na kuzifanyia kazi kwa kina ili kuondoa migogoro katika sekta hiyo.

“Kukiwa na migongano kwa pande hizi mbili hatuwezi kwenda na ndio maana tunakaa pamoja ili kujua kuna kero gani katika sekta zetu za kukuza uchumi kwenye mkoa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa DKT. Christine Ishengoma aliishukuru TNBC kwa jitihada zake za kuunganisha sekta hizo mbili ili kuweza kufanya kazi pamoja lengo likiwa ni kuendeleza mkoa wake.

“Mimi niseme kwamba TNBC wanajitahidi sana katika kutuunganisha, naomba waendelee na kazi hiyo ya kujenga nchi,” alisema Dk. Ishengoma.

Alisema mkoa wake una vivutio vingi vya uwekezaji na kuwa kinachotakiwa ni kuwekewa mazingira bora ya kufanya biashara ili wawekezaji wengi wawekeze Iringa kwani kwa kufanya hivyo mkoa utaweza kukua kiuchumi.

“Tuna utalii, kilimo pamoja na ufugaji hivi vyote ni vivutio vikubwa sana vya uwekezaji,” aliongeza.

Aidha aliwataka watendaji kuacha urasimu usiokuwa wa lazima kwani unakwamisha juhudi za serikali za kuondoa umasikini kupitia uwekezaji hasa pale mwekezaji anapohitaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

“Mimi nashanga sana mwekezaji anaweza kuzungushwa karibu mwaka mzima kwa kitu cha siku nne mpaka tano naomba tubadilike,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.


Mwisho

Wednesday, August 6, 2014

Watanzania wahamasishwa kujitolea, uzalendo kupata maendeleo

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mercy Sila (katikati) akizungumza na baadhi ya wajumbe waliofanya ziara nchini Korea kujifunza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji kipya cha maendeleo cha Saemaul Undong hivi karibuni jana wilayani humo.  Kulia ni mlezi wa Umoja huo, Mchungaji Joshua Lee na Mshauri wa umoja huo Bw. Mohamed Dolla.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mercy Sila (kushoto) akizungumza na wajumbe waliofanya ziara nchini Korea kujifunza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji kipya cha maendeleo cha Saemaul Undong hivi karibuni jana wilayani Mkuranga.  Kulia ni mlezi wa Umoja huo, Mchungaji Joshua Lee na Mshauri wa umoja huo Bw. Mohamed Dolla.
Mlezi wa umoja wa wajumbe waliofanya ziara nchini Korea kujifunza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji kipya cha maendeleo cha Saemaul Undong nchini Korea, Mch. Joshua Lee akizungumza jambo na wajumbe, Mohamed Dolla (kushoto) na Mwajuma Kingwande (katikati) walipotembelea eneo ambapo patajengwa daraja kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga ili kutatua tatizo la mawasiliano kati ya kijiji cha Njia Nne na Nyamihimbo.
Na Mwandishi wetu, Mkuranga

Kujitolea na uzalendo kwa nchi vimetajwa kama nyenzo muhimu za maendeleo kwa taifa la Tanzania.

Ushauri huo umetolewa na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Bi. Mercy Sila aliyekuwa anaongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika uchaguzi wa viongozi wa wajumbe waliotembelea kijiji cha maendeleo cha mfano cha Saemaul Undong nchini Korea ya Kusini hivi karibuni.

Bi. Sila alisema watanzania wakiamua wanaweza kuendelea na ndio msingi mkubwa wa kuleta maendeleo popote pale, hasa watu wanapohamasishwa kufanya kazi kwa umoja nguvu na msihikamano wa kweli.

“Suala la kimaendeleo si la viongozi bali ni wananchi wenyewe,” alisema Bi Sila.

Aliongeza kuwa Wakorea wamefanikiwa na kupiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na nidhamu ya hali ya juu katika kufanya kazi kwa kujitolea hivyo ni jukumu la viongozi kutoa hamasa kwa wananchi kulijua hilo.

“Tumeenda Korea tumeona wenzetu waklivyo kuambali, maendeleo yao yametokana na wananchi kupewa hamasa na kuona nchi ni ya kwao na si mtu kutoka nje” aliongeza

Alisisitiza kuwa umoja waliouwanzisha katika wilaya ya Mkuranga unapaswa kuwa wa kitaifa kwani ni jambo kubwa na la msingi kuona vijiji vinakua kimaendeleo hasa kwa wananchi wenyewe kuweka nguvu zao mbele.

“Wananchi wa kawaida Korea hawahitaji fedha kwanza, wamefundishwa namna ya kujitolea kujenga Taifa lao,”alisisitiza.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema vijiji vya Mfulu Mwambao pamoja na Njia Nne ndio vimefanywa vijiji vya mfano katika harakati hizo za kuleta maendeleo ya kweli na hilo limetokana na baadhi yao kwenda nchini Korea kujifunza namna watu wanavyofanya kazi kwa kujitolea.

“Wananchi wangu katika vijiji hivyo wameanza kuelewa na hii ni kutokana na baadhi yao kwenda korea kujifunza,” alisema.

Wananchi hao walienda katika moja ya maeneo ya mfano nchini humo na kijionea jinsi watu walivyojitolea katika kufanya kazi na kujenga nchi yao.

“kutokana na hali hiyo huu umoja wetu wa huku tulionzisha tutauita Saemaul Undong Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake, mlezi wa umoja huo,  Saemaul Undong, Mchungaji Joshua Lee alisema watanzania ni watu wenye utajiri mkubwa hivyo wanatakiwa kuhamasishwa ili kuweza kupata matunda zaidi ya utajiri huo.

“hakuna ambacho hakipo hapa, ni watu kuhamasishwa kufanya kazi ili wawe na maono ya mbali,” alisema.

Aliongeza kuwa huu ni wakati wa watanzania kuweka uzalendo mbele, kufanya kazi kwa kujitolea zaidi pasipo kudai fedha mara kwa mara na kwa kufanya hivyo wanaweza kuwa kama wakorea katika miaka ijayo.

Katika Uchaguzi huo wa umoja wa wajumbe waliotembelea nchini Korea uliwachagua Mkuu wa Wilaya Mstaafu wa Wilaya ya Mkuranga Bw. Henry Clemens kuwa Mwenyekiti, Bw. Gaudence Kayombo kuwa makamu Mwenyekiti, Apolinary Rutaga katibu na Mwajuma Kingwande kuwa mweka hazina huku Bw. Mohamed Dolla akiwa mshauri wa umoja huo.


Mwisho