Monday, May 5, 2014

Ole Naiko apigia debe Mfuko wa mitaji wa wafanyabiashara(Mkoba)

Mlezi wa  Asasi ya Diana Women Empowerment Organization ambaye pia Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emanuel Ole Naiko kati akifungua semina ya mafunzo ya wajasiriamali ambao ni wanachama wa asasi hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mwenyekiti wa taifa wa asasi hiyo, Bi. Farida Khakoo na kushoto ni Katibu wa Taifa wa asasi hiyo, Bi. Joyce Singano.
Mlezi wa  Asasi ya Diana Women Empowerment Organizationambaye pia Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emanuel Ole Naiko kulia akiangalia kazi za mikono zinazotengenezwa na wajasiriamali ambao ni wanachama wa asasi hiyo  na kushoto ni Mwenyekti wa asasi hiyo taifa, Bi. Farida Khakoo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mfuko wa Mitaji ya Wafanyabiashara (Mkoba Private Equity Fund) uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete  hivi karibuni umeelezwa kuwa ni kimbilio kubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika kupata mitaji ya kukuza biashara zao.

Mlezi wa Asasi ya Diana Women Empowerment Organization ambaye pia ni Balozi wa Heshima wa nchi ya Botswana hapa Tanzania, Mhandisi Emmanuel Ole Naiko ameuelezea mfuko huo kama kimbilio la wajasiriamali.

“Uzinduzi wa mfuko huo umekuja wakati mwafaka kwa vile Tanzania tuna tatizo kwa wajasiriamali wadogo na wakati kupata mitaji ya kuendeleza na kukuza shughuli zao za kibiashara,” Bw. Ole Naiko aliyasema hayo mwishoni mwa wiki  jijini Dar es Salaam wakati akifungua  semina ya siku moja ya wajasirimali wa asasi hiyo.

Alisema serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),  imejitahidi kuweka mifumo mizuri ya sheria kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje lakini tatizo lililpo ni namna ya kupata mitaji kwa vile benki zina masharti magumu ya kupata mikopo.

“Kwa  kweli uzinduzi wa mfuko huo utasaidia sana kuchochea shughuli za biashara na ujasiriamali hapa nchini kwa vile kutakuwa na sehemu ya kupata mitaji,” alisema na kuongeza kuwa ni vyema wajasiriamali wakachangamkia fursa za kuwepo kwa mfuko huo.

Bw. Ole Naiko  aliwaasa pia  waanasemina hao kuzingatia mafunzo ya ujasiriamali na kwamba elimu, mbinu na maarifa  wanayoyapata wakayatumie  kwa vitendo ili kuzidi kuendeleza kibiashara.

“Mafanikio katika biashara yanaanza kwa mtu mwenyewe na hakuna mtu anayeweza kuja kuwaendeleza katika biashara zenu bila  wenyewe kujitambua na kujiongezea maarifa”aliongeza kusema.

Aliwaasa wajasiriamali hao kuzitumie fursa zinazojitokeza za kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara kwa faida yao na taifa kwa ujumla kwani mchango wa wajasiriliamali ni mkubwa sana.
 Mwenyekiti wa Taifa wa Asasi hiyo, Bi. Farida Khakoo alisema semina hiyo ilishirikisha wanasemina 40 ambao ni wajasiriamali na wanachama wa asasi hiyo.

“Asasi yetu inalea watoto yatima, walemavu na wajane na ina wanachama ambao ni wajasiriamali,”alisema.
Alisema semina hiyo inalenga kuwafundisha wajasiriamali hao nanma ya kutunza kumbukumbu za hesabu za biashara zao katika vitabu ili waweze kuendesha vema biashara.

Naye mwanachma na mjasirimali wa asasi hiyo,Bi. Constance Chandende alisema semina hiyo itamwezesha kupata ujuzi zaidi wa kuendesha shughuli zake za ujasiriamali na kufikia malengo.

“Mimi biashara yangu ni ya kusindika matunda yakiwemo ya pilipili mbuzi, michaichai, maembe na mbilimbi,”alisema.

Alisema wanawake wengine nchini wasikae bila kazi bali yajiingize katika biashara mabalimbali ili waweze kuwa na mchango katika familia.

Mwisho.


Friday, May 2, 2014

Wafanyabiashara DRC wahamasishwa kutumia ofisi mpya za TPA Lubumbashi

Na Mwandishi wetu, Lubumbashi
Serikali ya Tanzania imesema imedhamiria kuhakikisha wafanyabiashara toka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam wanapata huduma nzuri kwa faida ya nchi zote mbili.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amesema wakati wa uzinduzi wa ofisi ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, DRC kuwa wizara yake na bandari ya Dar es Salaam watahakikisha kuwa huduma za bandari zinasogezwa karibu na DRC.

“Nawahimiza wafanyabiashara wa DRC kutumia kwa ufanisi ofisi hii kwa faida ya jamii nzima ya nchi yao,” alisema.
Waziri alisema kuwa ofisi hizo mpya zitasaidia wafanyabiashara wa DRC kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.

“Wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.

Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.

Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara tokea Dar es Salaam hadi Lubumbashi kupitia Zambia kwa barabara zaidi ya kilometa 2000 kuangalia na kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC bandarini Dar es Salaam njiani wanaposafiri.

Ofisi ya Lubumbashi inalenga kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabishara hao zikiwemo ucheleweshaji, wizi, vikwazo visivyohusiana na kodi na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu.

“Juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa vikwazo na urasimu wote unaowakabili wafanyabiashara wa Congo unakwisha,” alifafanua Waziri.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba ambaye ni mmoja wa ujumbe wa Tanzania aliyesafiri na Waziri alisema hatua hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi zote mbili.

Aliishauri TPA kuhakikisha inaweka wafanyakazi wenye moyo na uadilifu katika ofisi hiyo mpya.

“Naishauri mamlaka hii iweke wafanyakazi wenye moyo na kazi, waadilifu na wazalendo kwa heshima ya nchi yetu,” alisema.

Makamu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Bw. Saidi Sauko amesifu hatua hiyo akisema kuwa itasaidia shirika lao kuongeza ufanisi wa kazi zao.
Shirika hilo linahusika sana katika kusafirisha mizigo ya DRC kupitia reli ya TAZARA.

Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.
Pamoja na maafisa wengine, ujumbe huo ulijumuisha pia maafisa waandamizi toka TPA, Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), Tanzania Railways Limited (TRL), TAZARA na wengine.

Mwisho.



Chiza aipa changamoto Bodi mpya ya RUBADA

Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) baada ya bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake mwishoni mwaka jana.
Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza( kulia) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA),Profesa Lucian Msambichaka (katikati)wakati alipokuwa akizindua bodi hiyo, kushoto ni Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Aloyce Masanja.
 Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
Wajumbe wa Bodi ya mpya ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) wamepewa changamoto ya kutimiza malengo yote waliyojiwekea katika kipindi chao cha miaka mitatu kwa kuongeza ufanisi zaidi wa mamlaka hiyo .

Waziri wa Kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alitoa changamoto hiyo jijini Dar es Salaamjana wakati akizindua bodi hiyo na kuwataka wajumbe wa bodi kufikia malengo waliyojiwekea na kuifanya RUBADA kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

“Ningependa kuona mnajiwekea malengo yenu na mnatimiza kwa wakati ili mtakapo maliza muda wenu muweze kusema mliiletea mafanikio mamlaka hii,”alisema Mhandisi Chiza.

Alisema wizara yake ina imani kubwa sana bodi hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Profesa Lucian Msambichaka ambaye ni miongoni mwa wachumi waliobobea hapa nchini.

Mbali ya Profesa Msambichaka, wajumbe  wengine katika bodi hiyo ni pamoja na Profesa Henry Mahoo, Mhandisi Bashir Mrindoko, Gaspar Luanda, Mhandisi Hosea Mbise, Mhandisi Raphael Dalluti, Dkt. Ben Moshi, Bi.Eline Sikazwe naBi. Nkuvililwa Simkanga.

Aliitaka bodi hiyo kuharakisha zoezi la upatakanaji wa sheria mpya ya mamlaka ili shughuli za uendelezaji bonde hilo zisiweze kukinzana na sheria nyingine.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa pia na Naibu waziri wa wizara hiyo, Bw. Godfrey Zambi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Raphael Daluti.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profsea Lucian Msambichaka alisema atahakikisha maagizo yaliyotolewa na waziri wa kilimo na ushirika yanatekelezwa ili kufikia malengo ya mamlaka.

“Ni lazima tutekeleze majukumu yetu na ninaamini bodi yetu ni nzuri na ina watu muhimu na wenye weledi mkubwa katika kutimiza majukumu,”alisema.

Alisema uongozi wake utahakikisha unachangua baadhi ya miradi na kuifanyia kazi ili bodi itakapomaliza kipindi chake iweze kuonyesha mafanikio yaliyopatikana.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw, Aloyce Masanja alisema uzinduzi wa bodi hiyo mpya anauchukulia kama ni chachu katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Sisi tumejipanga kushirikiana na bodi mpya katika kuhakikisha miradi inayokusudiwa ikiwemo ya Kilimo, na uzalishaji nishati ya umeme inafanikiwa,”alisema.

Alisisitiza kuwa shughuli kuu zinazofanywa na mamlaka ni pamoja na uhamasishaji ,uratibu na udhibiti wa mafuriko na usimamiaji wa shughuli za maendeleo kwenye Bonde la Mto Rufiji.

Alisema bonde hilo linaumihimu mkubwa kwa vile miradi yote ya Mpango wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) inapatika katika bode hilo na miradi yote iliyopo kwenye bonde ni sehemu ya kufikia mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Alisema bodi hiyo iliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Mwezi October mwaka 2013 na sasa imeziduliwa tayari kwa kuanza kufanya kazi rasmi kwa kushirikiana na menejimenti.

Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA ni taasisi ya serikali iliyopewa jukumu la kusimamia na utekelezaji wa shughuli za bonde hiyo.

Mwisho.