Monday, March 3, 2014

Wafanyabiashara watakiwa kuondoa vibanda vya biashara stendi ya Ubungo

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara wenye vibanda vya kukatia tiketi katika stendi ya Ubungo ambako Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) unaendelea, wametakiwa kuviondosha vibanda hivyo katika maeneo hayo ili kupisha ujenzi wa mradi huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne Sagini aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa wafanyabiashara hao wanatakiwa kuondoa vibanda vyao ili kupisha ujenzi wa mradi huo unaoendelea katika eneo hilo.
“Tunataka waondoe vibanda vyao katika eneo la Ubungo ili kupisha mradi unaoendelea uweze kukamilika kwa muda tulioupanga,” alisema Bw. Sagini.
Alisema wafanyabiashara hao walishalipwa fidia baada ya kufanyiwa tathimi lakini cha kushangaza bado wanaendelea kuwepo katika maeneo hayo na kusababisha mradi kutoendelea kwa kasi iliyokuwa inakusudiwa katika eneo hilo.
Alisema serikali ililipa Jiji la Dar es Salaam fedha kwa ajili ya kuwapatia fidia wao, na uongozi wa jiji ulifanya hivyo na kila mtu alipata fidia hiyo.
 “Kwa vile uongozi wa Jiji la Dar es Salaam uliwalipa fidia wenye vibanda,sasa wanapaswa kusimamia zoezi hili na kuwaondosha kabisa hao waliobaki kwa sababu hawastahili kuwepo tena katika maeneo haya,”aliongeza kusema Bw. Sagini.
Alisema dhamira ya serikali ni kuona mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa kwa sababu ukichelewa kwa makosa ya hapa nchini, serikali itaingia gharama ya kumlipa mkandarasi kwa kuchelewesha mradi.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka inayosimamia mradi huo ya DART,Bi. Asteria Mlambo alisema maeneo yote ya Ubungo wakati mradi unaanza kulikuwa na majengo mbalimbali zikiwemo hoteli na vibanda vya kukatia tiketi.
“Maeneo haya yote yameshafidiwa thamani ya Tsh milioni 260 kupisha mradi  kuendelea kujengwa,” aliongeza kusema, Bi. Mlambo.
Hivi karibuni DART iliingia mkataba na kampuni ya washauri itakayofanya kazi ya kupatikana watoa huduma muhimu kwa mradi huo unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kampuni hiyo ya REBEL Group ya Uholanzi kushinda zabuni na kushindanishwa na kampuni nyingine.
Mradi huu unalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa foleni na msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Barabara zinazohusika na awamu hii ni pamoja na kilomita 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi Morocco.

Mwisho


Wadau wasifu maboresho ya bandari ya Dar

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wadau na watumiaji mbalimbali wa Bandari ya Dar es Salaam wamepongeza maboresho yaliyofanywa na serikali katika bandari hiyo na kuelezea kuridhishwa na ufanisi wa huduma zinanavyo tolewa kwa sasa.
Mbali ya kupongeza maboresho hayo, wadau wameridhishwa na hatua mbalimbali ambazo serikali kupitia Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA)kuanza kufanya kazi masaa 24.
“Hii ni dalili njema kwa uchumi wa nchi yetu na nchi jirani,” Mkurugenzi wa kampuni inayojishughulisha na huduma za mizigo bandarini hapo, Reindeer Investment Limited, Bw. Mlimuka Luhanga aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Bw. Luhanga alisema juhudi za kuiimarisha bandari ya Dar es Salaam zinaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani katika eneo hili la Afrika na kusema kuwa kama kazi hiyo ikifanywa vyema itakuwa faida kubwa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje pamoja na nchi kwa ujumla.
Hata hivyo Bw. Luhanga ameipa changamoto serikali kuimarisha zaidi usafiri wa reli nchini kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kusafirisha bidhaa zinazopakuliwa bandarini na kuzisafirisha sehemu husika.
“Kwa kutumia barabara tu hatuwezi kufanikisha kusafirisha mizigo yote kwa wakati na vilevle barabara zetu hazitadumu kwa muda mrefu hivyo miundombinu ya reli itasaidia sana kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi jirani,” alisema mkurugenzi huyo.
Naye Bw.Safari Kazimoto ambaye anajishughulisha na shughuli ya uingizaji magari kutoka nje na kuyauza amesifu maboresho ya huduma ya bandari na kusema yamerudisha imani kubwa kwa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam.
“Kwa miezi ya karibuni biashara yangu imeimarika kutokana na ufanisi katika bandari na vilevile imepunguza msongamano na kuleta imani kwa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam,”alisisitiza Bw. Kazimoto.
Kwa upande wake Bw. Pierre Nzwagiba ambaye ni mfanyabiashara kutoka Congo DRC, aliwaambia waandishi wa habari kuwa bandari ya Dar es Salaam ni bandari kubwa  na inauwezo mkubwa wa kupitisha mizigo mingi na maboresho yaliyofanywa hivi karibuni yataimarisha biashara.
“Naipongeza TPA kwa kuchukua hatua za makusudi kwa makusudi kuhakikisha imani ya watumiaji wa bandari hii wanarudi na wanaendelea kutumia huduma kama kawaida,” alisema Nzwagiba.
Raia huyo wa Congo DRC, ameitaka serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika miundombinu na uboreshaji wa huduma bandarini na kutoridhika na maboresho hayo tu.
Katika miaka ya hivi karibuni pamekuwepo na mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, TPA pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa bandari ya Dar es Salaam inatoa huduma bora kwa wateja wa hapa nchini pamoja na wale wan chi jirani.
Kutokana na mikakati hiyo pamekuwepo na ongezeko la shehena, tija katika kuhudumia shehena na meli zinazotumia bandari hiyo, na kupungua kwa msongamano wa meli.
Pia kumekuwepo na punguzo kubwa la mrundikano wa mizigo na kufanikiwa kukomesha vitendo vya upotevu wa mizigo na wizi kwa kiasi kikubwa.
Kwa mfano, kwa upande wa mapato, mwaka 2012/13 wastani wa Tshs bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia 14.3 ukilinganisha na Tsh. bilioni 325.3 mwaka 2011/12.
Katika mapato hayo, bandari bila ya makusanyo ya TICTS, ilikusanya Tsh.bilioni 324.5 mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.9, ikilinganishwa na mapato ya Tsh.bilioni 272.9 mwaka 2011/12.

Mwisho.



TIC yapongeza maendeleo kilimo cha miwa EcoEnergy

Meneja mradi wa kilimo cha miwa cha Kampuni ya EcoEnergy Tanzania Limited, Bw. William Burston akieleza maendeleo ya mradi huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Bi.Juliet Kairuki (blauzi nyeusi) pamoja na wafanyabiashara kutoka mji wa Vallejo Jimbo la California Marekani ambao walikuwa katika ujumbe uliokuwa ukiongozwa na Meya wa Mji huo, Bw. Osby Davis.  Walitembelea shamba hilo kujionea mfano halisi wa uwekezaji hapa nchini.
Maneja wa Shamba la Kampuni ya EcoEnergy, Bw. Andre’ Fred’ Herbe( wa pili kushoto) akielezea jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji nchini (TIC),Bi Juliet Kairuki (wa pili kulia) maendeleo ya shamba la miwa la kampuni ya EcoEnergy lilopo Bagamoyo hivi karibuni.  Wa kwanza kulia ni Meya  wa mji wa Vallejo uliopo katika Jimbo la California Marekani, Bw. Osby Davis na Meneja mradi wa Kampuni ya EcoEnergy, Bw. William Burston (kushoto).  Bi. Kairuki na wafanyabiashara hao walitembelea shamba hilo kujionea mfano halisi wa uwekezaji hapa nchini.
Na Mwandishi Wetu, Pwani
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesifu Kampuni  ya EcoEnergy Tanzania kuwa shughuli zake za Kilimo zinazolenga kupunguza tatizo la uhaba wa sukari na nishati ya umeme.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa kituo hicho, Bi Juliet Kairuki alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea shamba kubwa la miwa linalomilikiwa na kampuni hiyo katika bonde la mto Ruvu.
“Tumekuja kujionea maendeleo ya shamaba hili ambalo ni moja ya miradi mikubwa ya kilimo hapa nchini,” alisema Bi Kairuki.
Shamba hilo linazalisha zao la miwa kwa nia ya kuzalisha sukari na kutengezea nishati ya umeme.
Katika ziara hiyo aliambatana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka mji wa Vallejo ulipo jimbo la California Marekani ambao walikuwa wakiongozwa na Meya wao, Bw.Osby Davis.
Alisema wafanyabiashara hao walitembezwa katika mradi wa shamaba hilo la miwa kwa nia ya kuwavutia kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Kilimo.
 “Mradi huu unatarajia kuajiri watu wengi,”aliongeza kusema Bi. Kairuki akielezea zaidi mradi huo.
Aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa serikali inatoa vivutio mbalimbali vya uwekezaji, na kufanikiwa kwa mradi wa shamaba hilo la miwa ni matokeo ya vivutio hivyo.
Alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa taifa kwa kuwa utasaidia kuleta ujuzi na teknolojia kuhusiana na kilimo cha kisasa cha miwa hapa nchini.
Naye Meya Davis alisifu harakati zinazofanywa na Tanzania katika kuinua Kilimo na shughuli nyingine za biashara na uchumi zinazofanyika hapa nchini.
“Tumejionea mradi huu mradi huu wa miwa unavyoendelea...ni matumaini yangu umewavutia wafanyabiashara toka Vallejo kuja kuwekeza Bagamoyo,” alisema.
Katika hatua nyingine Meya huyo pia alitumia ziara hiyo kutembelea shule za Msingi Majengo na Mbaruku za mji wa Bagamoyo na kutoa zawadi mbalimbali.
“Tunatambua kuwa njia kuu ya kupata maendeleo na kukuza uchumi ni kuwekeza katika elimu,” alisema na kuongeza kuwa wameamua kusaidia kuwekeza katika watoto hao.
Alisema misaada hiyo waliyoitoa ni sehemu ndogo tu, kwa kuwa mji wa Bagamoyo na Vallejo ni marafiki, hivyo uongozi wa mji huo unalenga kuleta maendelea zaidi ya kiuchumi na kijamii katika mji wa Bagamoyo.
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kiliandaa ziara ya ujumbe wa wafanyabiashara kutoka mji wa Vallejo ambao walitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika mji wa Bagamoyo.

Mwisho.