Monday, October 7, 2013

Kambi ya vijana ya kilimo Mkongo ilete ukombozi -Kikwete

Rais Jakaya Kikwete akimsalimia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja wakati akiwasili kuzindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa Mkongo wilayani Rufiji hivi karibuni. Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Profesa Lucian Msambichaka na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bw. Yamungu Kayandabila (kwanza kushoto).
Na Mwandishi wetu, Pwani
Rais Jakaya Kikwete amesema kambi ya vijana ya kilimo na Maarifa Mkongo iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani iwe moja ya mifano hai ya kuondoa umaskini na kuwakomboa wananchi kivipato.
Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo alipokuwa akifungua rasmi kambi hyo iliyobuniwa na Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) hivi karibuni wilayani Rufiji.
“Umasikini wa watu wetu utaondoka kupitia jitihada kama hizi zenye dhamira ya kuwakomboa kivipato,” alisema na kuongeza kuwa vijana hao wakitumia ujuzi waliopata kwa vitendo watabadilika kimaisha na watakuwa mfano kwa jamii yote.
Alisema kambi hiyo ni nzuri kwa vijana na haina budi kutoa mafunzo ya kilimo ambayo yatawawezesha kwenda kujiajiri na siyo kusubiri ajira ili wakaeneze ujuzi huo katika maeneo wanayotoka.
Kambi ya vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo ni moja ya njia za utekelezaji wa azma ya serikali ya kuleta mapinduzi ya kijani Kupitia mpango wa Kilimo Kwanza.
Kambi hiyo imeanza na vijana 50, kati ya hao wavulana wakiwa 36 na wasichana 14.
Rais alisisitiza kwamba vijana hao watakapomaliza mafunzo yao wawezeshwe ili watakaporudi katika vijiji vyao wakatumie ujuzi walioupata kwa vitendo kupata fedha.
“Hawa wakitoka hapa wasiachwe tu, mkiwaacha muda mfupi mtawakuta wanacheza pool…hivyo ufanyike utaratibu maalumu  wa kuwawezesha kwa usimamizi maalumu ili mashamba yao yakawe kivutio kwa watu wengine kupenda kilimo,” alisema.
Akitoa mfano alisema mazao nyanya, tikitimaji na matango ya shamba darasa ya kambi hiyo yana soko kubwa, hivyo watakapomaliza mafunzo hayo wakatumie ujuzi huo kulima mazao hayo ili kufanikiwa.
Pia aliitaka RUBADA na Wizara ya Kilimo na Ushirika kuhakikisha wanatafuta aina bora ya mbegu inayozaa mazao mengi ili vijana hao wakafurahie kazi hiyo na kuwavutia wenzao na jamii nzima.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja alisema kambo hiyo pia ni utekelezaji wa mpango wa kukuza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ambao unalenga kuleta mapinduzi ya haraka ya kilimo kikanda unaojumuisha jitihada na nguvu za pamoja za wadau mbalimbali.
RUBADA inatekeleza mpango huu kwa mtindo wa “Hub and Spoke” ambapo mwekezaji mkubwa wa ndani au wa nje anakuwa “Hub” na wakulima wadogo wanakuwa “Spoke” wote kwa pamoja wakisukuma gurudumu la maendeleo.
Akifafanua zaidi alisema mtindo huu unahusu kuanzisha kambi za vijana kwa kila eneo lenye mwekezaji mkubwa katika bonde zima la mto Rufiji linaloanzia mkoa wa Pwani, Morogoro, Iringa, Mbeya, sehemu ya Dodoma, Singida, Ruvuma na Lindi.
Bw. Masanja alisema kufuatana na mkakati sa SAGCOT uliobainisha kongani sita za Rufiji, Kilombero, Ihemi, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga; RUBADA, imeandaa mpango kabambe wa utekelezaji ambao utashirikisha vijana katika kila kongani.
“Kwa mwaka huu wa fedha, tunategemea kuwa na vituo vitano vya vijana katika kilimo na maarifa na kila kituo kitakuwa na vijana wasiopungua 300 ambao watapata mafunzo katika kipindi cha mwaka mmoja,” alisema.
Vituo hivyo vya vijana vitakuwa na majukumu ya kutoa mafunzo kuhusiana na utekelezaji wa kilimo bora chenye tija; kuongeza thamani mazao; matumizi ya vifaa vya kisasa; utekelezaji wa kilimo bora bila uharibifu wa mazingira; kuandaa andiko la mradi ili kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha na uundaji wa vikundi vya ushirika.
Kwa mujibu wa Bw. Masanja, mafunzo katika kambi hizo yatajikita katika maeneo makuu matatu yakihusisha uzalishaji wa mazo ya kilimo kwa wingi na yenye thamani kubwa hasa mazao ya bustani, mboga mboga na matunda; ufugaji wa kisasa wa ng’ombe na kuku na ufugaji wa samaki pamoja na ujasiriamali.
“RUBADA inatarajia kuzalisha vijana 600 kutoka kituo cha Mkongo hadi 2015 ambao watakuwa na utaalamu na ujuzi wa kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa,” alisema Mkurugenzi huyo.
Kilimo ni moja ya sekta zinazolengwa katika mikakati mbalimbali ya serikali katika mapinduzi ya kiuchumi na kufikia malengo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Kulingana na sense ya watu ya 2012, asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana.
Mwisho  

Saturday, October 5, 2013

Tanzania yaongeza juhudi kujenga mazingira bora ya biashara mipakani

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye akizungumza katika warsha ya kutathimini, kuongeza kasi na ubora katika Utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini jana jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Bw. Mbarak Abudulwakil (katikati)
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka akizungumza katika warsha ya kutathimini, kuongeza kasi na ubora katika Utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini jana jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imewahakikishia wafanyabiashara kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya biashara za mipakani ili kuvutia uwekezaji kwa ustawi wa jamii na uchumi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa swala hilo ni la muhimu na la msingi sana kama nchi inataka kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufikia maendeleo endelevu.
“Katika utaratibu wa soko huria ni wajibu wa serikali kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuleta ustawi na ushindani kwa sekta binafsi kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Alisema sekta binafsi inapokuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji inasaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na upatakanaji wa mapato ya serikali.
Alifafanua kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yanapokuwa magumu wanaoteseka ni wananchi wa kawaida kutokana na kukosa ajira na huduma muhimu.
Alisema pamoja na kwamba mazingira yaliyopo bado hayakidhi vigezo vya kimataifa, serikali inashirikiana na sekta binafsi katika kuboresha mazingira hayo.
 Alisema maboresho yaliyofanywa yamesaidia biashara na uwekezaji kufanya vizuri na hatua zaidi zinachukuliwa za kuboresha sera na sheria ili hata uchumi uweze kukua kwa asilimia 10 kwa mwaka.
Alisema azma hiyo ni ya dhati katika kuhakikisha mazingira yanakuwa wezeshi, na kuchochea wananchi kutumia fursa na rasirimali zilizopo kuchangia uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alisema mpango wa kuimarisha biashara mipakani ukizingatiwa utasaidia sana kuimarisha biashara na uwekezaji.
Mpango huo unawaleta pamoja wataalamu kutoka sekta ya umma na wawakilishi wa sekta binafsi kuchambua, kupanga na kutathmini hatua za kuboresha mazingira ya biashara katika maeneo ya mipaka.
Alisema lengo lake ni kuainisha vikwazo na hatua ambazo wizara na taasisi za serikali zinahitajika kuchukua kwa kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kuboresha mazingira hayo.
Akitoa mfano alisema biashara za mipakani imekuwa na vikwazo vingi ambavyo vinajadiliwa kupata ufumbuzi ili bidhaa kutoka bandari ya Dar es Salaam ziweze kwenda nje ya Tanzania bila vikwazo.
Alisema Wizara ya Mambo ya Ndani imejitahidi kurekebisha mazingira hayo na sasa warsha hii itasaidi sana kupata ufumbuzi zaidi wa biashara za mipakani.
Alisema sekta binafsi, imeunda vikosi kazi vinne ambavyo kazi yake ni kufuatilia utekelezaji wa mpango huo kuanzia kuanzisha na Kufunga Biashara, Biashara za Mipakani, Upatikanaji wa Vibali vya Ujenzi na Kuandikisha Raslimali. 
Alisema tathmini iliyofanyka Machi mwaka 2012 na mshauri elekezi kuhusu utekelezaji wa mpango huo inaonyesha kuwa kati ya hatua 193 zilizotakiwa kuchukuliwa, ni 43 tu ikiwa sawa na asilimia 22 tu zilizotekelezwa kikamilifu.
Alisema taarifa za Benki dunia zinazotolewa kila mwaka zinaonyesha Tanzania bado ipo chini katika kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji ukilinganisha na nchi 185 duniani.
Alisema Rais wa Jakaya Kikwete alianzisha mchakato wa Tanzania kuboresha nafasi yake kimataifa katika wepesi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 120, hadi chini ya 100 ifikapo 2011.
Alisema pia hadi kufikia mwaka huu Tanzania bado haijapiga hatua ya kuridhisha na kwamba bado kuna changamoto zinazohitaji utelekezaji kufikia hatua hiyo.
Washa hiyo ya siku mbili ilishirikisha washiriki toka sekta ya umma na binafsi kufanya tathimini, kuongeza kasi na ubora katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Mwisho

Thursday, October 3, 2013

Kikwete anatarajiwa kufungua kambi ya kilimo ya vijana Rufiji kesho

Na Mwandishi watu, Dar es Salaam
Rais Jakaya Kikwete anatarajia kufungua rasmi kambi yaya kwanza vijana katika kilimo na maarifa ya Mkongo iliyo katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Jumamosi wiki hii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja ambao ndio waanzilishi wa kambi hiyo, uanzishwaji wa kambi hiyo ni moja ya utekelezaji wa kuwashirikisha vijana kwenye kilimo.
“Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa mageuzi katika sekta ya kilimo wenye lengo la kuwabadilisha kimtazamo vijana ili kukubali na kuona kuwa kilimo kinalipa,” aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Bw. Masanja alisema kuwa mpango huu unawajengea uwezo vijana ili waweze kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za kilimo na unalenga katika maeneo yaliyochaguliwa kwa ajili ya Matokeo Makubwa Sasa kwenye bonde la mto Rufiji.
Pia alisema ni utekelezaji wa mpango wa kukuza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ambao unalenga kuleta mapinduzi ya haraka ya kilimo kikanda unaojumuisha jitihada na nguvu za pamoja za wadau mbalimbali.
RUBADA inatekeleza mpango huu kwa mtindo wa “Hub and Spoke” ambapo mwekezaji mkubwa wa ndani au wa nje anakuwa “Hub” na wakulima wadogo wanakuwa “Spoke” wote kwa pamoja wakisukuma gurudumu la maendeleo.
Akifafanua zaidi alisema mtindo huu unahusu kuanzisha kambi za vijana kwa kila eneo lenye mwekezaji mkubwa katika bonde zima la mto Rufiji linaloanzia mkoa wa Pwani, Morogoro, Iringa, Mbeya, sehemu ya Dodoma, Singida, Ruvuma na Lindi.
Bw. Masanja alisema kufuatana na mkakati sa SAGCOT uliobainisha kongani sita za Rufiji, Kilombero, Ihemi, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga; RUBADA, imeandaa mpango kabambe wa utekelezaji ambao utashirikisha vijana katika kila kongani.
“Kwa mwaka huu wa fedha, tunategemea kuwa na vituo vitano vya vijana katika kilimo na maarifa na kila kituo kitakuwa na vijana wasiopungua 300 ambao watapata mafunzo katika kipindi cha mwaka mmoja,” alisema.
Vituo hivyo vya vijana vitakuwa na majukumu ya kutoa mafunzo kuhusiana na utekelezaji wa kilimo bora chenye tija; kuongeza thamani mazao; matumizi ya vifaa vya kisasa; utekelezaji wa kilimo bora bila uharibifu wa mazingira; kuandaa andiko la mradi ili kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha na uundaji wa vikundi vya ushirika.
Kwa mujibu wa Bw. Masanja, mafunzo katika kambi hizo yatajikita katika maeneo makuu matatu yakihusisha uzalishaji wa mazo ya kilimo kwa wingi na yenye thamani kubwa hasa mazao ya bustani, mboga mboga na matunda; ufugaji wa kisasa wa ng’ombe na kuku na ufugaji wa samaki pamoja na ujasiriamali.
Kwa kuanzia, kambi ya Mkongo inaanza na vijana 50 lakini ikiwa na lengo la kuchukua vijana 300 kwa mara moja ili kituo kiweze kufikia malengo yake.